Michezo mwishoni mwa wiki | Michezo | DW | 17.10.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Michezo mwishoni mwa wiki

Nusu-finali ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika jumamosi hii.

Klinsmann na B.Munich

Klinsmann na B.Munich

Baada ya kinyanganyiro cha kati ya wiki kanda ya Ulaya,Amerika Kusini na Asia kuania tiketi za kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini,Ligi mashuhuri zinarudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii: Leo ni nsu-finali ya champions-League-kombe la klabu bingwa barani Afrika.Enyimba ya Nigeria,inawaonya leo mabingwa Al Ahly wa Misri, kwamba itakiona leo kilichomtoa kanga manyoya.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani,viongozi wa Ligi Hamburg,wamepania kutetea uongozi wao kileleni kesho wakiwakaribisha Schalke nyumbani.

Chelsea ina miadi na Middelsbrough wakati Liverpool inaikaribisha Wigan Athletics katika changamoto za Premier League nchini Uingereza.

Swali : ni timu gani mbili mwishoe, zitakata tiketi zao kwa finali na kuliwakilisha baadae mjini Tokyo bara la Afrika katika kombe la klabu bingwa za dunia ?

Stephen Worgu wa Enyimba adai klabu yake itawasangaza leo wamisri tena katika zizi lao na ni wao watakaotoropka na tiketi ya finali ya kombe hili la klabu bingwa.

Lakini, Enyimba ilimudu sare ya 0:0 nyumbani Aba, nchini Nigeria wiki 2 nyuma inawezaji leo kudai itatamba ugenini mjini Cairo ? Ishara zote zabainisha hivyo ni vishindo vya darini tu vya Enyimba , vitakavyoishia sakafuni mjini Cairo.Kwani, mabingwa mara 5 wa kombe hili Al Ahly,hawataacha tiketi nyengine ya finali kuwaponyoka.

Ufunguo wa ushindi wa Enyimba unaegemea mkakati kwamba ili washinde nyumbani leo,Al Ahly lazima wahujumu na wakihujumu, waweza wakafanya makosa langoni mwao.

Mashabiki wa Al Ahly hatahivyo, wanaamini sana kwamba taji lao la 6 la klabu bingwa liko njiani kuingia kabatini mwao.Hii inafuatia kumudu tu sare na Etoile du Sahel ya Tunisia 0-0.

Enyimba inasaka ushindi wao wa kwanza kabisa dhidi ya Al Ahly baada ya kulazwa nyumbani bao 1:0 na halafu ugenini 2-1 katika kombe hili 2005.Hatahivyo, Enyimba ikimudu tena sare nyumbani leo itaitoa Al Ahly na kutoroka na tiketi ya finali ya kombe hili.

Katika nusu-finali ya pili, makamo-bingwa 1998 Dynamo ya Zimbabwe ,wamedhihirika kuwa si rahisi kufua dafu mbele yao.Hatahivyo, walizabwa bao 1:0 nyumbani na Contonsport ya Kameroun.Watoto hao wa Harare lakini wanajivunia ushindi wao dhidi ya Etoile du sahel mjiniSousse na ASEC Mimosas ya Ivory Coast mjini Abidjan.Dynamo yaweza kutamba leo tena mbele ya Contonsport,ingawa jogoo la shamba haliwiki mjini.ikigombea kuwa timu ya kwanza kucheza finali ya kombe hili la klabu bingwa kutoka Kameroun tangu zama za Cannon Yaounde ilipotwaa taji 1980,Contonsport,inaahidi kuwatimua nje leo Dynamo na kuwarudisha Harare mikono mitupu.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, macho yatakodolewa kesho changamoto kati ya viongozi wa Ligi-Hamburg na Schalke.Hamburg inaongoza Ligi ya Ujerumani kwa pointi 3 ikifuastwa nyuma na Hoffenheim iliopanda tu msimu huu daraja ya kwanza.Schalke inamtegemea kumteremsha uwanjani mshambulizi wao Kevin kuranyi ambae jumamosi iliopita aliachamkono timu ya Taifa ya Ujerumani.

Cologne ilioanza kuja kwa meno ya juu baada ya kuitimua nje Borussia Monchengladbach hivi majuzi, inatapia pointi 3 nyengine nyumbani leo kutoka Energie Cottbus.

Bayern Munich, mabingwa wakiongozwa na kocha wao Klinsmann hawamudu kupepesuka tena hii leo nyumbani mwa Karlsruhe.

Frankfurt inacheza na Leverkusen wakati Hoffenheim inaitembelea Hannover.Werder Bremen iko nyumbani ikiikaribisha leo Borussia Dortmund.Berlin inacheza na Stuttgart .

Ama katika premier League-Ligi ya uingereza, viongozi wa Ligi Chelsea na Liverpool wote wanarudi leo uwanjani: Chelsea ina miadi na Middelsbrough wakati Liverpool inaikaribisha nyumbani Wigan Athletic.Manchester United inapambana leo na West Bromwich.Arsenal inacheza na Everton wakati Aston Vila inaumana na Portsmouth.