Mgomo wa Sudan ′wafuiya′ | Matukio ya Afrika | DW | 19.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

SUDAN

Mgomo wa Sudan 'wafuiya'

Mgomo wa wa upinzani nchini Sudan kupinga kupandishwa kwa bei za bidhaa muhimu umeshindwa kufikia lengo lake, baada ya mabasi kuonekana yakiwasafirisha wafanyakazi kwenda maofisini na shule zikisalia wazi. 

Mgomo huo wa siku moja ni sehemu ya vuguvugu la uasi wa umma lililoanzishwa dhidi ya uamuzi wa serikali wa mwezi Novemba kupandisha bei za mafuta, hatua ambayo imesababisha ongezeko la bei za bidhaa nyingine, zikiwemo dawa.

Lakini raia wengi wameamkia kazini na usafiri wa magari mjini Khartoum umeendelea kuwa kama kawaida. 

Wakati wa maandalizi ya mgomo huo, makundi ya wanaharakati, wasanii, wanasheria, walimu na wanafamasia walitumia mitandao ya kijamii kuhamaisha uungaji mkono hatua hiyo, baada ya mgomo kama huo wa siku tatu mwezi uliyopita kuitikiwa kwa hisia mchanganyiko. 

Siku ya tarehe 12 Disemba, Rais Omar Hassan al-Bashir aliapa kuyasambaratisha maandamano yoyote ya kuipinga serikali kama ilivyofanyika miaka mitatu iliyopita.

Serikali ya Khartoum imelazimika kupunguza taratibu za ruzuku ya mafuta tangu 2011, wakati Sudan Kusini ilipojitenga na kuondoka na karibu robo tatu ya hifadhi ya mafuta ya Sudan iliyokuwa imeungana.