Mgombea wa upinzani wa Guinea-Bissau ashinda urais | Matukio ya Afrika | DW | 02.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mgombea wa upinzani wa Guinea-Bissau ashinda urais

Tume ya uchaguzi ya Guinea-Bissau imemtangaza kiongozi wa upinzani Umaro Sissoco Embalo kuwa mshindi wa uchaguzi wa duru ya pili ya urais huku chama tawala cha PAIGC kikiyapinga matokeo.

Embalo ameshinda kwa asilimia 54 ya kura kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa na tume ya uchaguzi huku mgombea wa chama tawala cha PAIGC Domingos Simoes Pereira akipata asilimia 46 ya kura katika uchaguzi wa duru ya pili uliofanyika siku ya Jumapili.

Baada ya kutangazwa na rais wa tume ya uchaguzi, Embalo aliwaeleza wafuasi wake kwamba atakuwa "rais wa taifa la mshikamano" na kutoa wito kwa taifa kuungana naye.

"Guinea Bissau sasa ina rais wa Jamhuri kuanzia Januari mosi ambaye ni mimi! Umaro Sissoco Embalo. Guinea Bissau haitakuwa tena nchi mnayoifahamu, nchi ambayo kila mtu anafanya anachojiskia. Hilo limekwisha. Guinea Bissau litakuwa taifa linaloheshimika,  watu wataheshimiana na hakuna mtu atakayetengwa," amesema Embalo.

Domingos Simoes Pereira (DW/B. Darame)

Mgombea wa chama tawala Domingos Simoes Pereira

Wafuasi wake waliupokea ushindi wake na kusherehekea katika hoteli iliyokuwa na ulinzi mkali wa polisi katika mji mkuu wa Bissau, ambako matokeo yalitangazwa. Mgombea wa chama tawala Pereira, ameyakataa matokeo hayo na kuahidi kuyapinga mahakamani. 

"Watu wa Guinea Bissau wanastahili kuelezwa matokeo dhahiri ambayo yanalingana na kile kilichotekelzwa katika sanduku la kura"

Embalo mwenye umri wa miaka 47 anachukua mikoba ya Jose Mario Vaz ambaye aliingia madarakani mwaka 2014 kwa matumiani ya kurejesha utulivu katika taifa hilo ambalo hukabiliwa na mapinduzi tangu lijipatie uhuru kutoka Ureno mwaka 1974. Muhula wa Vaz ulitawaliwa na mapambano ya kisiasa, bunge lisilofanya kazi na ufisadi.

Kama shauri la Pereira la kupinga matokeo litashindwa, Embalo ambaye amehudumu kama waziri mkuu chini ya utawala wa Vaz kati ya mwaka 2016-2018, atakabiliwa na jukumu zito la kushughulikia mkwamo wa muda mrefu wa kisiasa pamoja na kuleta mageuzi katika taifa hilo la Afrika magharibi lenye jumla ya wakaazi milioni 1.6.

Hata hivyo inahofiwa kuwa malalamiko ya Pereira yanaweza kusababisha vurugu zaidi za kisiasa ambazo zimelikumba taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni. Guinea-Bissau imekabiliwa na karibu majaribio 9 ya mapinduzi tangu ijipatie uhuru wake mwaka 1974.

reuters/AFP