1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meta, TikTok na X, wabanwa kuhusu usalama mtandaoni

Sylvia Mwehozi
1 Februari 2024

Wakurugenzi wa makampuni makubwa ya teknolojia duniani ikiwemo Meta, TikTok na X, walikabiliwa na maswali mazito kutoka kwa wabunge wa Marekani juu ya kitisho kinachowakabili watoto na vijana mitandaoni.

https://p.dw.com/p/4bvpJ
Marekani | Nembo ya kampuni mama ya mtandao wa Facebook Meta
Nembo ya kampuni mama ya mtandao wa Facebook MetaPicha: Arnd Wiegmann/REUTERS

Wakurugenzi hao waliitwa mbele ya kamati ya bunge ya mahakama kujadili madhara ya teknolojia na mgogoro wa unyanyasaji kingono kwa watoto mitandaoni.

Wakurugenzi hao wanakabiliwa na wimbi la hasira, kwa kushindwa kuwalinda watoto kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa wazi wa kingono na vijana kujiua.

Mkurugenzi wa kampuni ya Meta, Mark Zuckerberg alilazimika kuomba radhi kwa familia za wahanga wa matukio hayo waliofika kusikiliza kikao hicho, wakati alipokabiliwa na maswali makali.

Soma pia:Mashambulizi ya mtandaoni yatibuwa dunia

Meta, ambayo inamiliki mitandao maarufu duniani ya Facebook na Instagram, ilisema itazuia ujumbe wa moja kwa moja unaotumwa kwa vijana wadogo na watu wasiowafahamu.