1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato waanza kumpata waziri mkuu Japan

Sekione Kitojo
8 Septemba 2020

Chama tawala nchini Japan leo(08.09.2020) kinaanzisha rasmi mbio za kumpata mrithi wa waziri mkuu Shinzo Abe, ambapo mshirika wake wa karibu Yoshihide Suga akiongoza kundi la watia nia lakini akiwa mbele yao mno.

https://p.dw.com/p/3i8WU
Yoshihide Suga, japanischer Chefkabinettssekretär
Yoshihide SugaPicha: Yoshikazu Tsuno/AFP/Getty Images

Suga katibu mkuu  wa  baraza  la  mawaziri, mwenye umri wa miaka 71 mtoto wa mkulima, tayari  amepata uungwaji  mkono wa makundi muhimu katika  chama  cha  Liberal Democratic kabla ya  uchaguzi wa  kiongozi  wa  chama  hapo Septemba  14. 

Lakini Suga hagombei bila  kupingwa, ambapo waziri maarufu wa zamani wa ulinzi  na  mkuu  wa  sera  za  chama  anagombea dhidi yake.

Japan Premirminister Shinzo Abe erklärt Rücktritt
Waziri mkuu anayeondoka madarakani Shinzo AbePicha: Reuters/F. Robichon

Wakati chama  cha  LDP kina  wingi  wa  kutosha  bungeni, mshindi wa  mbio  hizo ana  hakika  ya  kushinda  kura  bungeni  hapo Septemba  16 na  kuteuliwa  kuwa  waziri  mkuu  mpya  wa  nchi hiyo.

Mbio za kumpata  waziri mkuu  mpya  kutoka  chama  cha  LDP zilianza, baada  ya  waziri mkuu  aliyehudumu  kwa  kipindi  kirefu nchini  Japan Shinzo Abe, ghafla  alitangaza  mwishoni  mwa  mwezi Agosti  kuwa  atajiuzulu kutokana  na  sababu  za  kiafya.

Kuna uvumi  kwamba  kiongozi  mpya  pia anaweza  kuitisha uchaguzi  wa  mapema  kuvutia uungwaji  mkono  wa  umma.

Leo asubuhi , wawakilishi wa Suga na  mahasimu  wake, waziri wa zamani wa  ulinzi Shigeru Ishiba na  mkuu  wa  sera  za  chama Fumio kishida, rasmi wamejiandikisha  kuwa  wagombea.

Uchaguzi na mapema

Wagombea  wanatarajiwa  kutoa hotuba na  kuwa na  mkutano wa pamoja na  waandishi  habari  baadaye leo.

Japan LDP-Programmchef Fumio Kishida in Tokio
Mkuu wa sera za chama cha LDP Fumio KishidaPicha: Reuters/Kim Kyung-Hoon

Pia kutakuwa  na  midahalo miwili , licha  ya kwamba  upigaji  kura utakuwa wa  wabunge wa  chama  cha  LDP pekee  na wawakilishi watatu  wa  chama  kutoka kila  jimbo la Japan  katika  majimbo 47. Kura pana  zaidi  itakayojumuisha wanachama  wote haitafanyika, ambapo maafisa  wanasema  itachukua  muda  mrefu  zaidi kutayarisha.

Yeyote atakayechukua  uongozi  wa  ofisi  hiyo  ya  juu  kabisa katika  uongozi  nchini  Japan  atakabiliwa  na  changamoto  kadhaa, kuanzia  janga  la  virusi vya  corona  pamoja na kuuweka  vizuri uchumi  wa nchi  hiyo  na kuhakikisha  michezo  ya  Olimpiki  ya Tokyo  iliyoahirishwa  inafanyika.

hakuna  miongoni  mwa  wagombea  hao  watatu  anayeonekana kutoa  uwanja  wa  sera ambao  utatofautiana  kwa  kiasi  kikubwa kutoka  zile  za  Abe, ambapo Yoshihide  Suga amesema  wazi kwamba  anapanga  kuendeleza mipango  ya  waziri  mkuu anayeondoka  madarakani.

Japan Verteidigungsminister Shigeru Ishiba
Waziri wa ulinzi wa Japan Shigeru IshibaPicha: AP

"Nimeamua  kugombea katika uchaguzi wa chama cha  Liberal democratic LDP. Naahidi kufuata sera ambazo waziri mkuu Abe amejitolea mwili na  moyo  wake kuzisukuma mbele. Na ili kuzisogeza mbele  zaidi, nina nia ya kujitoa kuzitekeleza."

Ishiba na Kishida wote wamezungumzia  haja ya kuhakikisha  kuwa kichocheo uchumi  kilichotolewa baada ya mzozo wa  virusi  vya corona  vinalenga wale wenye uhitaji. Ishiba ambaye ni mfanyakazi wa zamani wa benki , mwenye umri wa miaka 63 ni  maarufu kwa wapiga kura  na  mara  kadhaa amekuwa akionekana kuwa chaguo la wapiga kura  kabla ya kujiuzulu kwa Abe.