Mazungumzo ya Sudan Kusini mashakani | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya Sudan Kusini mashakani

Wasuluhishi wa mzozo wa Sudan Kusini wanasema haiko wazi iwapo waasi watakutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana na serikali ya nchi hiyo na hiyo kuvuruga matumaini ya kukomesha kwa haraka mapigano ya kikabila nchini humo.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.

Mazungumzo hayo yanayofanyika katika nchi jirani ya Ethiopia tayari yamekuwa yakicheleweshwa mara kwa mara na kuanza vibaya. Wajumbe wa pande mbili zinazohasimiana wamekutana na wasuluhishi kutoka jumuiya ya kiserikali ya ushirikiano wa maendeleo wa kanda IGAD kwa siku ya pili Jumamosi lakini hawakukutana pamoja.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia Dina Mufti amesema bado wanashughulikia kukamililisha agenda ya mazungumzo hayo ambayo ndio itakayojadiliwa.

Alipoulizwa wakati gani pande hizo mbili zitakutana ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters "Hatuwezi kutabiri. Wanalishughulikia jambo hilo."Wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia hapo awali ilisema mazungumzo hayo yataanza Jumamosi.

Machar alaumu wawakilishi wa Kiir

Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar.

Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar.

Akizungumza katika mtandao wake wa Twitter baada ya kushindwa kukubaliana juu ya agenda mpizani wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ambaye alikuwa makamo wake wa rais hapo zamani Riek Machar amesema wamejitolea kwa ajili ya mazungumzo hayo ya amani ambapo maoni ya pande zote mbili yanaheshimiwa. Amesema "Upande Salva Kiir hauko tayari kulikubali hilo."

Kuendelea kwa mapambano zaidi hapo Ijumaa kati ya vikosi vya serikali ya Kiir vya SPLA na waasi walio tiifu kwa Machar kumeashiria kwamba usitishaji wa mapigano unaopiganiwa kufanikishwa na mataifa yanayopakana na nchi hiyo bado ni safari ndefu.

Mataifa makubwa ya magharibi na yale ya kanda ambayo mengi yao yaliunga mkono mazungumzo yaliopelekea Sudan Kusini kuwa uhuru kutoka Sudan hapo mwaka 2011 yamekuwa yakishinikiza kufikiwa kwa makubaliano kwa kuhofia kwamba mapigano mapya yanaweza kugeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuiyumbisha Afrika mashariki nzima.

Mapigano hayo tayari yameuwa watu zaidi ya 1,000 na kuwafanya wengine 200,000 kuyakimbia makaazi yao pamoja na kuteteresha masoko ya mafuta.

Waasi waelekea Juba ?

Vikosi vya serikali vikipiga doria mjini Juba ,(02.01.2014).

Vikosi vya serikali vikipiga doria mjini Juba ,(02.01.2014).

Msemaji wa waasi katika jimbo la kaskazini la Unity ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba vikosi vya waasi vimekuwa vikiisogelea Juba juu ya kwamba hakuna uthibitisho huru wa habari hizo na SPLA imekuwa ikizitupilia mbali repoti kama hizo katika kipindi cha wiki moja iliopita.

Sudan Kusini inaendelea kubakia kuwa mojawapo ya nchi zenye maendeleo duni kabisa barani Afrika licha ya kuwa na akiba kubwa ya mafuta ambapo imekadiriwa na kampuni ya mafuta ya BP kuwa ni ya tatu kwa ukubwa katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa uko katika mchakato wa kuongeza vikosi vyake Sudan Kusini katika juhudi za kuzuwiya kupamba moto kwa ghasia za umwagaji damu.

Umoja wa Mataifa waimarisha kikosi

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo (UNMISS) kimesema kimepokea askari polisi wa ziada 230 wa Bangladesh wakiwa na silaha kutoka kikosi chake kilioko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Askari polisi wa Bangladesh wa kikosi cha Umoja wa Mataifa wakiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juba. (31.12.2013).

Askari polisi wa Bangladesh wa kikosi cha Umoja wa Mataifa wakiwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juba. (31.12.2013).

Joseph Contreras msemaji wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kutoka Juba kwamba askari hao wamewekwa Juba,Bor na katika mji mkuu wa jimbo la Upper Nile wa Malakal na tayari wameanza kazi kikamilifu.

Contreras ameongeza kusema "Tunataraji kupokea kabla ya tarehe 15 Januari askari polisi wa Umoja wa Mataifa waliopewa mafunzo maalum kutoka Nepal ambao wanatumika kwa shughuli nyengine za kulinda amani huko Liberia."

Kikosi cha Umoja wa Mataifa kilioko Sudan Kusini hivi sasa kina wanajeshi kama 7,000 wenye silaha,bado kinasubiri kuwasili kwa wanajeshi wengine wa ziada wa kulinda amani 5,500 na washauri wa polisi walioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi iliopita.

Katika ishara ya hali kuzidi kuwa mbaya Marekani hapo Ijumaa imewataka wafanyakaziu wake zaidi pamoja na raia wake wengine kuondoka Sudan Kusini.

Mazungumzo ya Ethiopia yalikuwa yamepangwa kulenga wakati gani usitishaji wa mapigano unapaswa kuanza na usimamiwe vipi.Vikosi vya SPLA na waasi wote wamesema wanakusudia kuweka chini silaha zao.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri : Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com