1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndia

Mawaziri wa nje wa G20 waombwa kuwa na umoja

Lilian Mtono
2 Machi 2023

Waziri mkuu wa India Narendra Modi amewarai mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la mataifa ya G20 kuwa na msimamo wa pamoja katika masuala ya kiulimwengu.

https://p.dw.com/p/4O9QY
Indien | Narendra Modi
Picha: Indranil Mukherjee/AFP/Getty Images

India ambayo ndiyo inashikilia urais wa kundi hilo ni miongoni mwa mataifa yaliyokataa kulaani uvamizi huo wa Urusi nchini Ukraine na kushinikiza suluhu ya kidiplomasia. 

Amesema "Tunakutana katika wakati ambapo ulimwengu umegawanyika sana. Kama mawaziri wa mambo ya nje, ni kawaida kwamba majadiliano yenu yanaweza kuathiriwa na mivutano ya siasa za kimaeneo. Sote tuna misimamo yetu na mitazamo yetu juu ya jinsi mivutano hii inavyopaswa kutatuliwa. Hata hivyo, kama nchi zinazoongoza kiuchumi duniani, pia tunawajibika kwa wale ambao hawako katika chumba hiki."

Waziri mkuu Narendra Modi ameongeza kupitia hotuba yake iliyorekodiwa kwamba katika kipindi cha miaka michache iliyopita wote wameshuhudia mizozo katika masuala ya kifedha, mabadiliko ya tabianchi, majanga, ugaidi na vita, hali inayodhihirisha kwamba serikali nyingi ulimwenguni zilishindwa kusimama imara.

Soma Zaidi: Vita vya Ukraine vyaugubika mkutano wa mawaziri wa G20

Kassachstan Blinken in Astana
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken ametoa mwito kwa mara nyingine kwa Urusi kuondoka Ukraine.Picha: Olivier Douliery/REUTERS

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, amesema mkutano huo wa G20 umevurugwa kwa mara nyingine na suala la vita visivyo na msingi wowote vya Urusi nchini Ukraine na kuongeza kuwa nchi hizo zinalazimika kuendelea kuitolea mwito Urusi kuondoka Ukraine.

Aidha, Blinken amerudia shinikizo la kuitaka Moscow kuingia upya makubaliano yaliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ya kuruhusu mauzo ya nafaka za Ukraine, ambayo muda wake unaisha mwezi huu. Anatoa mwito huu, wakati Sergei Lavrov, waziri wa mambo ya nje ya Urusi akiyashutumu vikali mataifa ya magharibi kwa kile alichoita kuuzika bila ya aibu mkakati wa nafaka kwenye Bahari Nyeusi uliowezesha uuzwaji nje wa bidhaa za kilimo za Ukraine zinazotokea kwenye bandari zake za kusini, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Novosti hii leo.

Soma Zaidi: Marekani yawatuhumu mawaziri wa Urusi kwa unyama Ukraine

Makubaliano hayo yaliingiwa upya mwezi Novemba, lakini mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alionya juu ya ugumu wa kufikiwa kwa makubaliano mengine kabla ya haya ya sasa kufikia ukomo Machi 18 mwaka huu.

Ukraine Besuch Meloni bei Selenskyj
Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesema ana imani India itafanikisha upatikanaji wa amani nchini Ukraine kwa njia ya mazungumzo.Picha: GLEB GARANICH/REUTERS

Katika hatua nyingine, waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni amesema leo kwamba ana matumaini kwamba India kama rais wa kundi hilo la G20 itafanikiwa kuratibu mpango wa kupatikana kwa amani nchini Ukraine. Meloni amewasili India hii leo kwa ziara ya siku mbili na kumwambia waziri mkuu Modi kwamba wanaamini India itachukua jukumu muhimu kabisa la kupatikana kwa amani na kusisitiza kwamba Italia inaunga mkono kikamilifu uhuru wa Kyiv.

Mkutano huo wa mawaziri hao wa mambo ya nje unafanyika siku chache baada ya mkutano uliowakutanisha mawaziri wa fedha wa kundi hilo la G20 ambao pia walijadili kwa kina vita vya nchini Ukraine. Mkutano huo ulimalizika kwa kutolewa waraka wa yaliyojadiliwa badala ya taarifa ya pamoja kutokana na kukosekana kwa makubaliano miongoni mwao juu ya kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Soma Zaidi: Mkutano wa G20 wamalizika bila makubaliano muhimu kuhusu vita vya Urusi na Ukraine

Mkutano huo unaohudhuriwa na wajumbe 40, unawakutanisha ana kwa ana kwa mara ya kwanza Blinken na Lavrov tangu mwezi Julai huku kukiwa hakuna matarajio ya wawili hao kufanya mazungumzo. Waziri wa mambo ya nje wa China, Qin Gang pia anahudhuria. Kwenye mkutano huo China na Urusi pia wameyakosoa vikali mataifa ya magharibi kwa kile walichoita uzushi na vitisho vinavyofanywa na mataifa hayo.