Mashambulizi mashariki mwa Congo yaendelea kutesa raia | Matukio ya Afrika | DW | 23.11.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mashambulizi mashariki mwa Congo yaendelea kutesa raia

Siku mbili baada ya wapiganaji wa kundi la uasi, CODECO, kushambulia kambi ya wakimbizi ya Drodro katika wilaya ya Djugu, wakimbizi pamoja na wakaazi wamekimbilia kijiji jirani cha Rho, ambako wanaishi katika hali mbaya.

Takribani wakimbizi laki moja waliopata hifadhi katika kijiji cha Rho, kilomita kumi na mbili hivi kutoka mji mdogo wa Drodro.

Wakizungumza na DW, wakimbizi hawa wamesema wanaishi katika mazingira magumu katika kambi ya Rho, kambi inayolindiwa usalama na jeshi la Tume ya Umoja wa Mataifa, Monusco. 

Mashambulizi ya Jumapili yalitokea hata baada ya wakaazi wa Drodro kuwataarifu viongozi wa jeshi kuhusu uwepo wa waasi. Kushindwa kwa jeshi katika kukabiliana na CODECO kabla ya kundi hilo kushambulia, kuchoma kambi na kuwauwa wakimbizi, kumekosolewa na mashirika ya kiraia ya Ituri, yanayoomba afutwe kazi kamanda wa jeshi wa Drodro.

DR Kongo UN-Soldaten in Djugu-Territorium | Ituri-Provinz nach Unruhen

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa

Hata hivyo, jeshi linasema limeimarisha ulinzi katika mji mdogo wa Drodro pamoja na viunga vyake, huku likiendesha operesheni za kuwafyeka waasi, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi katika mkoa wa Ituri, Jules Ngongo. Malalamiko ya wakaazi kwamba jeshi hilo halitendi wajibu wake ipasavyo, hayajapokelewa vizuri na jeshi, ambalo kupitia msemaji wake wa mkoa wa Ituri, Luteni Jules Ngongo, linatishia kuwatia nguvuni watu wanaoeneza chuki dhidi ya viongozi, wakati huu wa hali ya dharura.

"Mkongomani wote mkaazi wa Ituri anapashwa kuachana na kuunga mkono makundi ya uasi na kuwa na uhusiano mzuri na jeshi na katika kipindi hiki kuwa na imani na jeshi. Tunawatahadharisha watu wanaosambaza fununu, kukatisha tamaa wanajeshi na kusambaza chuki dhidi ya viongozi, wanaofanya hivyo wataadhibiwa na hiyo katika siku nne zitakazofuata."

Milio ya risasi imekuwa ikisikika katika viunga vya Rho, na hali ni ya wasiwasi katika kijiji hicho.