1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wa CODECO waingia mji wa Bunia DRC

John Kanyunyu/DW Beni4 Septemba 2020

Wakaazi wa mji wa Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri kaskazini mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wameamka leo na kuwakuta wanamgambo wa kundi la waasi wa CODECO wakiranda katika mitaa ya mji wao.

https://p.dw.com/p/3i1JO
DR Kongo UN-Soldaten in Djugu-Territorium | Ituri-Provinz nach Unruhen
Picha: AFP/S. Tounsi

Duru zinaarifu kuwa wanamgambo hao wamekwenda Bunia kushinikiza kuachiwa huru wenzao wanaoshikiliwa gerezani.

Hao ni mamia ya wanamgambo wa kundi la CODECO,walioingia leo katika mji wa Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri, wakiimba wimbo wa taifa, pembezoni mwa gereza kuu la Bunia, wanakotajwa kuwa walikuja kuwaondoa jela, wanachama wa kundi lao.

Uwepo wa wanamgambo hao wanaoshukiwa kufanya mauaji ya kila mara katika wilaya ya Djugu, umesababisha hofu kubwa miongoni mwa wakaazi, baadhi yao wakijificha majumbani, na wengine wakifuatilia kwa karibu hali inayojiri mjini, wakitaka kujua kinachofuata.

Katika kuwafariji wakaazi wa mji wake waliotiwa kiwewe na kuwaona uso kwa uso wanamgambo hao wa CODECO, meya wa Bunia Fimbo Lebiliye anawaeleza wakazi hao kinachoendelea kwa wakati huu.

"Walionesha nia ya kuja kusalimisha silaha zao kwa viongozi wa sekta ya operesheni. Askari jeshi wamejipanga sawasawa, na kunao pia askari polisi walioko katika eneo husika. Kunayo pia mazungumzo yanayoendelea, ilikuwaomba warudi katika eneo walikotokea na tatizo lao litashughulikiwa baadae. Hadi sasa hawajaonesha nia ya kushambulia. Tunatathmini hali, pale mazungumzo yakiendelea. Tunadhani kwamba tutafikia muhafaka." Amesema Fimbo Lebiliye.

Wanamgambo hao washinikiza wenzao walokamatwa kuachiwa huru
Wanamgambo hao washinikiza wenzao walokamatwa kuachiwa huruPicha: AFP/S. Tounsi

Mji wa Bunia wenye maelfu ya wakimbizi walioyahama makaazi yao kutoka wilaya ya Djugu, ambako ndiko waasi wa CODECO wanaendesha shughuli zao, na idadi kubwa ya wakimbizi hao ikiwa inatokea katika kabila la bahema, mmoja wa wazee wa kabila hilo John Kabwa Nduru, analaumu kitendo cha kuingia Bunia kwa wanamgambo wa CODECO wakiwa na silaha mkononi, pale akijiuliza hasa maana ya uwepo wa serikali pamoja na ujumbe wa Umoja wa mataifa katika mkoa wa Ituri.

Wanamgambo wa CODECO, wanashukiwa kuwauwa ma mia ya raia katika wilaya ya Djugu, na mauwaji hayo yameshachukuliwa na Umoja wa mataifa kuwa ni uhalifu wa kivita.

Na hadi tunatuma ripoti hii, hali bado ni ya wasiwasi katika mji wa Bunia,hasa karibu na gereza kuu la mji huo, ambako wamejipanga wanamgambo hao,  huku wakazi wengi wakijiuliza kitakachotokea ikiwa serikali haitawaachia huru wenzao.