1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yatangaza kukamata meli nyingine ya Iran

Iddi Ssessanga ape,afpe,rtre
23 Aprili 2026

Jeshi la Marekani limetangaza kukamata meli nyingine ya mafuta inayohusishwa na Iran katika Bahari ya Hindi, hatua inayozidi kuongeza mvutano huku vita ya kiuchumi ikiendelea licha ya kusitishwa kwa makabiliano.

https://p.dw.com/p/5CjNR
Bahari ya Kiarabu 2026 | Mwangamizi wa Marekani USS Spruance akizuia meli ya mizigo ya Iran M/V Touska
Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza Jeshi la Wanamaji kufyatua risasi na kuangamiza boti zinazoweka mabomu ya majini katika Mlango Bahari wa Hormuz.Picha: CENTCOM/Handout/REUTERS

Marekani imesema imekamata meli ya mafuta iitwayo , ikidai ilikuwa sehemu ya mtandao wa kusafirisha mafuta ya Iran kinyume cha vikwazo. Wizara ya Ulinzi, Pentagon, imesisitiza kuwa operesheni hizi zitaendelea duniani kote ili kuzuia mtiririko wa mapato kwa Tehran.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Iran nayo kukamata meli mbili za mizigo katika Mlango Bahari wa Hormuz, hali inayoashiria "kulipizana kisasi” kati ya pande hizo mbili katika bahari.

Wakati mvutano huo ukiongezeka, Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza hatua kali zaidi za kijeshi baharini. Amesema ameagiza jeshi la wanamaji la Marekani "kutumia risasi na kuangamiza” boti ndogo za Iran zitakazojaribu kuweka mabomu ya majini katika Mlango wa Hormuz.

Katika ujumbe wake, Trump alisema: "Hakutakuwa na kusita, tumeongeza operesheni za kusafisha mabomu ya majini katika njia hiyo muhimu.” Kauli hiyo inaashiria kuongezeka kwa hatari ya mapigano ya moja kwa moja baharini.

Hatua hiyo inakuja baada ya Iran kushambulia meli tatu za mizigo na kukamata mbili kati yake, huku Marekani nayo ikiendelea na operesheni za kukamata meli zinazohusishwa na Iran katika maeneo ya mbali kama Bahari ya Hindi.

Iran Mlango Bahari wa Hormuz 2026 | Walinzi wa Mapinduzi wa Iran wakamata meli za mizigo
Picha ya skrini kutoka video ya IRGC iliyotolewa Aprili 23, 2026, inaonyesha boti ya jeshi hilo ikishiriki katika operesheni ya kukamata meli katika Mlango Bahari wa HormuzPicha: IRIB TV/AFP

Pakistan yaendelea kuwa na matumaini ya kuwa mwenyeji

Katikati mwa hali hiyo ya vuta nikuvute, Pakistan imeendelea kuonyesha matumaini kuwa mazungumzo ya amani yanaweza kufanyika.

Maafisa wake wanasema bado wanaendelea na maandalizi ya usalama mjini Islamabad kwa uwezekano wa kupokea ujumbe wa Marekani na Iran

"Hatua za usalama kwa ajili ya uwezekano wa kuwasili kwa ujumbe wa pande mbili muhimu bado zipo hapa Islamabad, jambo linaloonyesha matumaini kwamba mji mkuu wa Pakistan bado unaweza kuwa mwenyeji wa duru ya pili ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran," alisema Ripota wa shirika la habari la Associated Press.

Pakistan ilikuwa imepanga kuwa mwenyeji wa duru nyingine ya mazungumzo,lakini Ikulu ya White House ilisitisha ziara iliyopangwa ya Makamu wa Rais JD Vance mjini Islamabad baada ya Tehran kukataa kupeleka wajumbe kwenye majadiliano hayo.

Maafisa wawili wa Pakistan walisema mamlaka nchini humo zitaendeleza mipangilio ya usalama mjini Islamabad endapo ujumbe wa Marekani na Iran utawasili. Iran imetambua urefushaji wa usitishaji vita lakini haikusema iwapo Tehran ilikuwa tayari kushiriki duru ya pili.

Iran inavyoweza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Marekani

Iran yatunisa misuli, Marekani yakaza mzingiro

Wakati huo huo, Iran imechapisha video za wanajeshi wake wakivamia meli baharini, na pia kutangaza kuanza kukusanya ushuru kwa meli zinazopita Hormuz, licha ya madai ya Rais Trump kwamba Marekani ina udhibiti kamili wa njia hiyo.

Ripoti zinaonyesha kuwa licha ya mzingiro wa jeshi la Marekani, baadhi ya mafuta ya Iran bado yanafanikiwa kutoka kupitia njia zisizo rasmi, huku zaidi ya mapipa milioni 10 yakiripotiwa kusafirishwa ndani ya kipindi kifupi.