Marekani yamshitaki Assange kwa kukiuka Sheria ya Upelelezi | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yamshitaki Assange kwa kukiuka Sheria ya Upelelezi

Marekani imemfungulia muasisi wa tovuti ya uvujishaji wa nyaraka za siri Wikileaks Julian Assange mashitaka ya kuvunja Sheria za Upelelezi kwa kuchapisha nyaraka za kijeshi na kidiplomasia mnamo mwaka wa 2010

Wizara hiyo imeorodhesha mashitaka 17 mapya dhidi ya Assange, ikimtuhumu kwa kumuagiza na kumsaidia mtalaamu wa ujasusi, Chelsea Manning, kuiba nyaraka za siri za Marekani, na pia kwa njia ya kiholela kuviweka hatarini vyanzo vya siri katika Mashariki ya Kati na China ambavyo vilitajwa kwenye nyaraka hizo.

Mashitaka hayo dhidi ya Assange, ambayo sasa ni 18 kwa jumla, yanapinga madai yake kuwa yeye alikuwa tu mchapishaji wa taarifa alizopokea kutoka kwa Manning, kitendo ambacho kinalindwa chini ya Kifungu cha Katiba ya Marekani kinachohakikisha uhuru wa habari.

Mashitaka mapya yanadai kuwa Assange alishirikiana wazi na Manning kuiba mamia kwa maelfu ya nyaraka za siri "na sababu ya kuamini kuwa taarifa hizo zingetumika kuidhuru Marekani au kulifaidi taifa la kigeni”.

Großbritannien Protest gegen schwedischen Haftbefehl gegen Assange (picture-alliance/dpa/D. Lipinski)

Maandamano nje ya mahakama wakati wa kesi ya Assange

Aidha pia yamesema Assange alikataa onyo la Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani mwaka wa 2010 kuondoa majina ya vyanzo vya wizara yake na vya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, Syria, Iraq, Iran na China, vyanzo inavyosema vilijumuisha wanahabari, viongozi wa kidini, watetezi wa haki za binaadamu na wapinzani wa kisiasa.

Naibu Mwanasheria Mkuu John Demers amesema wizara ya Mambo ya Kigeni inalichukulia kwa umuhimu mkubwa jukumu la wanahabari katika demokrasia ya Marekani. Lakini Julian Assange sio mwanahabari.

Assange, mzaliwa wa Australia mwenye umri wa miaka 47, kwa sasa yuko gerezani nchini Uingereza kwa kukosa kufika mahakamani, na anakabiliwa na ombi la Marekani la kumtaka asafirishwe Marekani wakati atapoachiliwa huru miezi 11 kutoka sasa.

Lakini haijabainika wazi kama serikali ya Uingereza itaheshimu ombi hilo, na mashitaka haya mapya huenda yakavuruga mpango huo. WikiLeaks umeyakosoa mashitaka hayo, ukisema yanawatishia wanahabari.

Mashirika ya kutetea vyombo vya habari pia yamelaani vikali. Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka limesema mashitaka hayo yanatoa kitisho cha moja kwa moja kwa uhuru wa vombo vya habari na uwanahabari wa upelelezi. Mashitaka hayo yanaongeza juhudi za serikali ya Marekani kuwakandamiza wavujishaji wa taarifa za usalama wa taifa. Wakati utawala wa awali wa rais Barack Obama iliwawinda wafichuaji, akiwemo Manning, ilionekana kuweka mstari kuhusu makundi ya uwazi kama vile WikiLeaks, ili kutoingia kwenye vita vya uhuru wa wanahabari. 

Lakini baada ya WikiLeaks kutoa mchango muhimu katika operesheni ya urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani 2016, kwa kuchapisha nyaraka zilizoibiwa na wadukuzi wa Urusi ambazo zilimharibia sifa mgombea wa Democratic Hillary Clinton, maafisa wa Marekani walianza kulionyesha kundi hilo kama linaloshirikiana na maadui wa Marekani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com