1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Marekani yafanikiwa kumuua kiongozi mkuu wa Al-Qaida

Mohammed Khelef
2 Agosti 2022

Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kwamba kiongozi wa kundi la al-Qaida, Ayman al-Zawahiri, ameuawa na mashambulizi ya ndege yasiyo rubani ya Marekani mjini Kabul, nchini Afghanistan, huku Saudi Arabia ikisifia.

https://p.dw.com/p/4EzWz
Al Kaida Anführer Aiman az Zawahiri
Picha: Mazhar Ali Khan/AP Photo/picture alliance

Akizungumzia kutokea Ikulu ya White House usiku wa kuamkia Jumanne (2 Agosti), Biden aliitaja operesheni iliyomuua Zawahiri mjini Kabul kwamba imetenda haki na italeta faraja kwa familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Mbali ya mashambulizi hayo ya Septemba 11, Biden ametumia sababu nyengine ya ziada kuhalalisha uamuzi wake wa kuamuru mauaji ya Zawahiri. "Alifanya video, zikiwemo za wiki za hivi karibuni, akiwataka wafuasi wake kuishambulia Marekani na washirika wetu. Sasa, haki imetendeka na kiongozi huyu wa kigaidi hayupo tena." Alisema.

Akielezea undani wa mashambulizi hayo ya ndege zisizo rubani yalivyofanyika, Biden alisema maafisa wa ujasusi wa nchi yake waliifuatilia nyumba ya Zawahiri katika mtaa mmoja wa Kabul, ambako alikuwa akijificha na familia yake, na baadaye yeye Biden akaidhinisha operesheni hiyo wiki iliyopita na ikatekelezwa juzi Jumapili. 

"Operesheni hii ilipangwa kwa uangalifu, na kwa kiwango kikubwa imepunguza madhara kwa raia wengine. Na wiki moja iliyopita, baada ya kushauriwa kwamba mazingira yalikuwa sahihi, nilitowa idhini ya mwisho ya kumpata, na operesheni imefanikiwa. Hakuna hata mtu mmoja wa familia yake aliyeumizwa na hakuna madhara yoyote kwa raia." Alisema Biden.

Kifo kwenye baraza

USA US-Präsident Joe Biden äußert sich zur Tötung des Al-Qaida-Führers Ayman al-Zawahiri
Rais Joe Biden akitangaza kuuawa kwa Ayman al-Zawahiri.Picha: Jim Watson/REUTERS

Kwa mujibu wa duru za kiusalama, Biden aliidhinisha mashambulizi hayo ya ndege zisizo rubani aina ya Hellfire siku ya tarehe 25 Julai wakati akiwa anaendelea kujiuguza maambukizo ya virusi vya korona, na kwamba Zawahiri aliuawa asubuhi ya Jumapili (Julai 31) akiwa amekaa kwenye baraza ya nyumba yake katika mtaa mmoja wa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Zawahiri ametajwa na Biden kwamba ndiye hasa aliyekuwa kiongozi wa kiongozi wa wakati huo wa al-Qaida, Osama bin Laden, na hivyo ni mshukiwa wa moja kwa moja wa mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani, ambayo kwa mara ya kwanza yalishuhudia taifa hilo kubwa kabisa duniani likishambuliwa ndani ya ardhi yake.

Saudi Arabia, nchi anayotokea Bin Laden aliyeuawa na Marekani mwaka 2011 nchini Pakistan, imesema kuwa imefurahishwa na tangazo la Rais Biden la kumlenga na kumuua kiongozi wa kundi la Al-Qaida, Zawahiri. 

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Saudia, mzaliwa huyo wa Misri, anachukuliwa kama mmoja kati ya viongozi wa ugaidi aliyepanga na kuongoza operesheni za kigaidi ndani ya Marekani, Saudi Arabia na mataifa mengine duniani.