Marekani kuisaidia Iraq kupamba na Al Qaeda | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani kuisaidia Iraq kupamba na Al Qaeda

Marekani itaisaidia Iraq katika mapambano yake dhidi ya wanamgambo wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda lakini haitotuma vikosi vyake nchini humo.Imesema hayo ni "mapambano yao".

Wapiganaji wa kikabila katika mji wa Ramadi.(04.01.2014).

Wapiganaji wa kikabila katika mji wa Ramadi.(04.01.2014).

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema Jumapili(05.01.2014) wakati akiondoka Jerusalem kuelekea Saudi Arabia na Jordan kwamba " Ndio wana utashi wa kuisaidia serikali halali na iliochaguliwa kuwashinda magaidi."

Kerry amesema watafanya kila wawezalo kuwasaidia lakini hawafikirii kurudi nchini humo au kutuma majeshi yao. Ameongeza kusema " Haya ni mapambano yao na watawasaidia katika mapambano hayo."

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amewaambia waandishi wa habari wanamgambo hao ni hatari kabisa katika kanda hiyo na unyama wao dhidi ya raia katika miji ya Fallujah na Ramadi na dhidi ya vikosi vya usalama uko wazi kwa kila mtu kuushuhudia duniani.

Mabomu yaripuka Baghdad

Vyombo vya habari nchini Iraq vimeripoti kwamba takriban wapiganaji hao 30 wa jihadi wameuawa na shambulio la anga lililofanywa na ndege ya serikali kwenye viunga vya mji wa Fallujah hapo Jumamosi.

Wakati vikosi vya serikali vikiizingira miji hiyo ilioko kwenye jimbo la magharibi la Anbar,wimbi jipya la mashambulizi limeukumba mji mkuu wa Iraq, Baghdad Jumapili, ambapo kiasi cha watu 20 wameuawa kaika miripuko ya mabomu.

Wanamgambo wa Al Qaeda wakipiga doria Fallujah. (01.01.2014).

Wanamgambo wa Al Qaeda wakipiga doria Fallujah. (01.01.2014).

Haya ni mashambulizi ya karibuni kabisa kufanywa na wanamgambo wa Kisunni, ambao wamekuwa wakipambana na vikosi vya serikali kwenye eneo la magharibi mwa nchi, wanakodhibiti miji hiyo miwili muhimu. Katika kiunga cha Shaab, kinachokaliwa na waumini wengi wa madhehebu ya Shia, magari mawili yaliyotegwa mabomu yaliripuka na kuwaua watu 10 na kuwajeruhi wengine 26. Bomu jengine kama hilo kwenye mji wa Sadr, limeua watu watano na kuwajeruhi 10, ambapo watatu wengine wameuawa katika kiunga cha Bab al-Muadham na wengine 13 kujeruhiwa. Mashambulizi haya yanatokea, huku jeshi la Iraq likisema linahitaji siku mbili ama tatu kuwang'oa wanamgambo wa kundi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Sham kutoka jimbo la Anbar.

Fallujah ni shwari

Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki.

Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki.

Wakaazi wa Fallujah wamesema hali ni shwari tokea Jumamosi usiku ambapo wanamgambo wanadhibiti eneo la kati kati ya mji huo.Mapigano ya hapa na pale yameripotiwa leo ndani na nje ya mji wa Ramadi ambao ulikuwa ngome kuu ya waasi wa madhehebu ya Sunni wakati wa vita vilivyoongozwa na Marekani. Wanamgambo wa Al Qaeda waliteka sehemu kubwa za miji hiyo yote miwili wiki iliopita na wamekuwa wakizima harakati za vikosi vya serikali kujipenyeza kwenye miji hiyo tokea wakati huo.

Hali ya mvutano katika jimbo la Anbar imezidi kuongezeka tokea Disemba 28 wakati vikosi vya usalama vya Iraq vilipomkamata mbunge wa Kisunni aliekuwa akitafutwa kwa madai ya kuhusika na vitendo vya kigaidi.Miezi miwili baadae serikali ilivunja kambi ya kupinga serikali iliowekwa na Wasunni na kuzusha mapambano na wanamgambo.

Ili kupunguza mvutano huo serikali inayoongozwa na Washia iliondowa wanajeshi wake kutoka miji hiyo.Wabunge wa Kisunni wanaliona jeshi kuwa ni kibaraka wa Waziri Mkuu Nouri al Maliki ambaye analitumia kuwaandama wapinzani wake na kuimarisha madaraka yake.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa watu 8,868 wameuawa nchini Iraq hapo mwaka 2013 hiyo ikiwa ni idadi kubwa ya maafa kwa mwaka kuwahi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com