Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 28.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri

Wahariri leo wanatoa maoni juu ya Ukraine,aliyoyasema Papa Francis na juu ya unyanyasaji wa watoto .Pia wanaizungumzia hotuba ya Rais Francois Hollande wa Ufaransa baada ya chama chake kushindwa vibaya

Rais Francois Hollande wa Ufaransa

Rais Francois Hollande wa Ufaransa

Mhariri wa gazeti la "Darmstädter Echo" anasema sasa yapo mambo mawili ya kuyatilia maanani katika juhudi za kuiokoa Ukarine.

Kwanza ni siasa ya Urusi ya kujiingiza na kuiyumbisha nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anasema Urusi inapaswa kuachana na sera hiyo na badala yake ijaribu kuwadhibiti waasi wanaoiunga mkono .Na katika upande mwingine, anasema mhariri wa gazeti la "Darmstädter Echo" ni Rais mpya wa Ukraine Poroshenko.Jee ataweza kuwafanya watu wa nchi yake waamini kwamba yapo manufaa makubwa zaidi katika kubakia katika nchi hiyo na kushirikiana na nchi za magharibi,kuliko kuegemea upande wa Urusi?

Hollande hakusema jipya
Mhariri wa gazeti la "Thuringische Landeszeitung" anazungumzia juu ya hotuba iliyotolewa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa baada ya chama chake cha wasoshalisti kuchakazwa vibaya na chama cha mrengo mkali wa kulia, katika uchaguzi wa bunge la Ulaya.

Mhariri huyo anasema kwamba macho yote yalikuwa yameelekezwa nchini Ufaransa kwa Rais Hollande. Lakini katika hotuba yake ya dakika tano,Rais huyo alimangamanga na vidokezo vile vile vinavyosikika kila siku badala ya kuzungumzia juu ya njia ya kuyasahihisha makosa. Njia hiyo itampeleka Hollande mahala ambako atamkuta kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia Marie Le Pen akimsubiri kama Rais wa Ufaransa.

Papa Francis azungumzia Useja katika kanisa
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis wiki hii ameyazungumzia masuala muhimu mawili yanayolihusu Kanisa hilo. Kwanza juu ya useja,yaani hali ya makasisi kuishi bila ya kuoa. Na pili juu ya uovu walioufanya makasisi kwa watoto.

Mhariri wa gazeti la "Passauer Neue Presse" anatilia maanani kwamba Baba Mtakatif Francis amesema useja, yaani hali ya makakasi kuishi bila ya kuoa siyo kanuni isiyoweza kubadilika. Kauli hiyo ni ya kuizingatia sana, kwa sababu mpaka sasa hakuna Kiongozi mwengine wa Kanisa katoliki aliewahi kulitamka jambo kama hilo. Bado haujapitishwa uamuzi lakini wote wanaamini kwamba wakati umefika wa kulitafakari suala hilo la useja.

Juu ya watoto kufanyiwa uovu na makasisi, gazeti la "Passauer Neue Presse" linasema Baba Mtakatifu ametoa kauli ya uwazi kwamba wahalifu hawataweza tena kujibanza ndani ya kuta za kanisa.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo