Maoni ya wahariri juu ya ukosefu wa ajira barani Ulaya | Magazetini | DW | 09.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya ukosefu wa ajira barani Ulaya

Wahariri wanaizungumzia ripoti juu ya hali ya kijamii barani Ulaya na pia wanatoa maoni juu ya mazingira ya Wakristo katika mabara ya Afrika na Asia

Wasiokuwa na kazi barani Ulaya waongezeka

Wasiokuwa na ajira barani Ulaya waongezeka

Kuhusu hali ya kijamii barani Ulaya,gazeti la "Nordwest-"linasema bara la Ulaya halijawahi kuwa na idadi kubwa sana ya watu wasiokuwa na kazi kama ilivyo sasa. Lakini mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba,siyo idadi tu ya watu hao inayosababisha wasiwasi.

Jambo la wasi wasi mkubwa ni kwamba bara la Ulaya limegawanyika katika pande mbili-upande wa Kaskazini ambao ni tajiri na upande wa kusini ambao ni masikini. Ni kweli kwamba nchi za kaskazini zimepeleka fedha katika nchi za kusini.Lakini njia hiyo haikusaidia. Kinachotakiwa ni mageuzi katika taratibu za uajiri-yaani kwenye soko la ajira.

Mhariri wa gazeti la"Neue Osnabrücker"pia anasisitiza kwamba njia ya kupeleka fedha katika nchi zenye matatizo ya madeni,haitasaidia,kulitatua tatizo laukosefu wa ajira katika nchi hizo.Mhariri huyo pia anasisitiza ulazima wa kufanyika mageuzi katika taratibu za uajiri.Anasema ingawa mabilioni ya Euro yamepelekwa katika nchi zenye matatizo ya madeni,idadi ya watu wasiokuwa na kazi imeongezeka hadi kufikia kiwango kisichokuwa na kifani katika kipindi cha miaka 20 iliyopita barani Ulaya.Lakini anasema Ujerumani imeonyesha njia ya matumaini.

Hatua ndefu za kuleta mageuzi kwenye soko la ajira zimeleta matunda nchini Ujerumani.Taratibu za uajiri, ikiwa pamoja na sera nzuri ya mishahara ndiyo msingi ulioifanya Ujerumani iweze kuwa nguvu ya kushindana na nchi zingine katika masoko ya biashara duniani lakini mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau" anaitahadharisha Ujerumani.

Anasema kwamba sehemu kubwa ya dunia imezama katika maji,na kwa hivyo itakuwa vigumu kwa Ujerumani kuendelea kuwa kavu kwa muda mrefu. Mhariri huyo anauliza "Jee nani atanunua bidhaa za Ujerumani ikiwa hana fedha"?

Kwa Ujerumani,masoko ya barani Asia ni kama kipuri tu.Soko muhimu kwa Ujerumani ni Ulaya ambako katika nchi nyingi idadi kubwa ya watu hawana kazi. Sasa ni juu ya Ujerumani kusaidia kuleta ustawi barani Ulaya kote.Bila ya hivyo,furaha itaendelea kuwa kama kanga ya kuazima nchini Ujerumani.

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linazungumzia vitisho vinavyowakbili wakristo duniani. Mhariri wa gazeti hilo anasema siasa kali na chuki dhidi ya wakristo zinaenea kama ugonjwa wa kuripuka barani Afrika na Asia. Na mapinduzi katika nchi za kiarabu yameifanya hali ya wakristo iwe ngumu.Mustakabal wa wakristo wa madhehebu ya Koptik upo mashakani nchini Misri kutokana na utawala wa kiislamu. Na hali siyo nzuri kwa wakristo wa Syria. Katika mazingira hayo haitakuwa sahihi kwa dunia kutazama kando .Lazima dunia ijali kinachotokea kwa wakristo katika nchi hizo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu