Maoni : Ujumbe kwa viongozi wa Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 31.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Maoni : Ujumbe kwa viongozi wa Afrika

Katika taifa la Afrika magharibi la Burkina Faso bunge limetiwa moto. Waandamanaji wamekuwa wakiandamana kwa siku kadhaa dhidi ya Rais Blaise Compaore hilo likiwa ni onyo kwa watawala wote wa Afrika.

Compaore ameingia madarakani katika koloni hilo la zamani la Ufaransa hapo mwaka 1987 kwa njia ya mapinduzi.Alimuuwa kiongozi mashuhuri Thomas Sankara ambaye aliziteka nyoyo za watu kwa unyenyekevu wake na msimamo wake wa kimapinduzi.

Baada ya kuuwawa kwa Sankara na wengine walioitwa "wasaliti",Compaore alijitawaza kama mlezi halisi wa "mapinduzi ya kidemokrasia ya wananchi". Lakini licha ya kuwa madarakani kwa miaka 27 aliendelea kutuhumiwa kuwa dikteta licha ya kuruhusu vyama vingi na vyombo vya habari nchini humo.Hapo mwaka 2000 aliruhusu katiba ifanyiwe marekebisho kwa mara ya kwanza ili aweze kuendelea kubakia madarakani.Mara kwa mara amekuwa akiyavunja kwa kutumia nguvu maandamano ya kisiasa na kijamii mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2011.

Mapinduzi ya katiba

Tokea mwaka jana licha ya kuwa mkuu wa nchi amekuwa pia akishikilia wadhifa wa waziri wa ulinzi.Lakini jaribio lake la kutaka kubadili tena katiba kumuwezesha kubakia madarakani kwa vipindi vyengine viwili safari hili limegonga mwamba.Wakosoaji wake wameliita jaribio hilo kuwa "mapinduzi ya katiba" yaliyotowa cheche iliyoliunguza bunge mjini Ouagadougou.

Uasi huu unatowa matumaini na ishara ya wazi kwamba muda wa Compaore umemalizika na kwamba siku za wakongwe wa Afrika kun'gan'gania madaraka milele zimemalizika.Wananchi wanapinga kuwepo kwa viongozi wa aina hiyo kama Compaore na ikibidi hata kwa kutumia nguvu.Marais wamekuwa wakizidi kun'gatuka kikatiba katika nchi nyingi za Kiafrika baada ya kushindwa katika uchaguzi au baada ya vipindi viwili madarakani.

Ilikuwa ni Benin katika nchi ndogo kuliko hata Burkina Faso ambapo hapo mwaka 1991 Mathieu Kerekou alipoweka mfano na alikuwa mtu wa kwanza barani Afrika kuachia madaraka badaa ya kushindwa uchaguzi, Kenneth Kaunda alionyesha hivyo nchini Zambia na nchini Msumbiji marais wawili tayari wamen'gatuka baada ya kumaliza vipindi viwili madarakani.Nchini Ghana hata kiongozi wa mapinduzi Jerry Rawlings alianzisha kipindi cha kuingia kwenye demokrasia.Nelson Mandela alitumikia kipindi kimoja nchini Afrika Kusini,Thabo Mbeki pia hakubakia kwa muda mrefu na rais wa sasa Jacob Zuma hatothubutu kukiuka katiba ya nchi hiyo.

Vuguvugu la mabadiliko Afrika

Waafrika hawakubali tena kufanywa wapumbavu wengi wao ni vijana wenye kujiamini ambao wameelimika vizuri kwa kupitia mtandao na mitandao ya kijamii na kuunganishwa vyema na dunia. Kwa wao zile hadithi za kishujaa wakati wa mapambano ya ukombozi zimepitwa na wakati.Viongozi wa muda mrefu wa baada ya utawala wa ukoloni kama Robert Mugabe wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka (90), Paul Biya wa Cameroon mwenye umri wa miaka (81),Jose Eduardo do Santos wa Angola mwenye umri wa miaka (72) au Theodor Obiang Ngwema wa Equatorial - Guinea ni mifano iliopitwa na wakati.

Lakini bado kiongozi kama Joseph Kabila wa Congo inaonekana hawakusoma alama za nyakati. Kabila amekuwepo madarakani tokea mwaka 2001 ikimaanisha kwamba mwaka 2016 kitakuwa kipindi chake cha mwisho. Lakini washirika wake wanaendelea kuandaa marekebisho ya katiba.Nchini Burundi Rais Piere Nkurunzinza anafikiria kipindi cha tatu madarakani ambapo ifikapo mwajka 2019 atakuwa tayari amekuwepo madarakani kwa miaka 14.Watu kama hawa wanacheza na moto!Afrika imebadilika.Enzi ya wakongwe kuendekeza nafsi zao kisiasa imemalizika.

Kwa hiyo leo hii jina la Burkina Faso kama nchi ya watu wenye busara linawakilisha sio tu nchi hiyo bali bara zima la Afrika.Yumkini Compaore akawa na jeshi linalomuunga mkono kwa mara nyegine tena lakini hakika sio wananchi.!

Claus Stäcker Mkuu wa Idara ya Lugha za Kiafrika ya DW.

Claus Stäcker Mkuu wa Idara ya Lugha za Kiafrika ya DW.

Mwandishi :Claus Stäcker /M.Dahman

Mhariri:Josephat Charo