1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ni pigo kwa imani katika tume ya uchaguzi

Daniel Gakuba
21 Desemba 2018

Kuahirishwa tena kwa uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni pigo kubwa kwa uaminifu katika mchakato huo, na kulingana na maoni ya Dirke Köpp wa DW, siku 7 ni chache mno kutatua matatizo yaliyotajwa.

https://p.dw.com/p/3ATFb
Demokratischen Republik Kongo | Wahlkommision |  Wahlautomat
Picha: DW/F. Quenum

Hatua hii inaondoa hata uaminifu mdogo ambao tume ya uchaguzi CENI ilibakiwa nao mbele ya umma. Siku nne kabla ya tarehe iliyopangwa uchaguzi huo, Desemba 23, imeahirisha uchaguzi wa rais, wabunge wa taifa na wa majimbo. Kwa mara ya tatu, kusema kweli rais alipaswa kuchaguliwa mwaka 2016. Lakini serikali na tume ya uchaguzi ambayo uhuru wake ni kwa jina tu, kila wakati walipata visingizio vya kuzuia uchaguzi.

Dirke Köpp Kommentarbild App

Na sasa, umeahirishwa tena kwa siku saba. Muda mfupi ajabu, ambao lakini umesababisha ghadhabu katika kambi ya upinzani na asasi za kiraia.

Mara hii, mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi, Corneille Nangaa ametoa sababu ya moto uliounguza ghala ya vifaa vya CENI tarehe 15.12.2018. Bado hakuna vifaa vilivyonunuliwa kuchukua nafasi ya vile vilivyoteketezwa na moto huo, ambavyo ni pamoja na mashine 8000 za kupigia kura.

Doa kubwa kwenye haiba ya Corneille Nangaa

Lakini siku moto huo uliporipuka, Corneille Nangaa alikuwa akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama kawaida. Leo hii anasema uchaguzi umeahirishwa kwa siku saba. Kuahirishwa tu, sio kusimamishwa. Kuchezacheza na maneno namna hii ndiko kunamfanya asiwe mtu a kuaminika.

Bila shaka, wapanga mkakati wa tume ya uchaguzi wamo katika hali ngumu; ikiwa wangeahirisha uchaguzi kwa zaidi ya siku saba, hali hiyo ingezusha uasi. Watu hawajasahau kwamba tayari waliahirisha uchaguzi mara mbili, na hawajasamehe. Wamechoka. Wakongo hukiita kipindi hiki cha utawala wa Joseph Kabila, baada ya mihula yake miwili, ''Utelezi.''

Kilichomshinda Kabila kwa miaka, tume haikiwezi kwa wiki moja

Kabila na serikali yake wamekataa msaada wote kutoka nje, kwa kutumia maneno makali. Amekataa msaada wa kipesa, wa kivifaa, wala waangalizi. Kwa kifupi, hataki uingiliaji. Maandalizi ya uchaguzi yanakwenda vibaya, kuna nakisi katika bajeti, vifaa vilichelewa kufika, au vilikosekana kabisa.

Katika muda wa siku saba za kuahirisha uchaguzi, pengine, karatasi za kupigia kura zitakuwa zimefika mahali zinapohitajika, pengine. Lakini maradhi ya Ebola, na ghasia za makundi ya uasi, havitaondoka katika muda huo. Kama tume ya uchaguzi ingekuwa yenye ukweli, ingeahirisha uchaguzi kwa miezi, sio kwa siku saba. Lakini kwa kuogopa athari zake, inapiga hatua fupi fupi, lakini hata mbinu hiyo, Wakongo wanaijua.

Siku saba haziwezi kuondoa matatizo ya Kongo ambayo tume ya uchaguzi imeayataja. Rais Joseph Kabila amekuwa madarakani kwa miaka 17 na hakuweza kuyatatua, tume haiwezi kuyasuluhisha kwa wiki moja.

Mwandishi: Dirke Köpp

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Grace Kabogo