Maoni: Deutsche Bank kikaangoni | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Majalada ya FinCen

Maoni: Deutsche Bank kikaangoni

Deutsche Bank imetajwa kwenye kashfa ya Majalada ya FinCen na kwenye maoni yake, Henrik Böhme, anasema benki hiyo imejikuta kwenye kashfa hii kwa kuwa iliacha misingi yake ya awali na kuelemea kwenye uroho na ufisadi.

"Kila kitu huanza na imani". Hivi ndivyo Deutsche Bank ilivyokuwa ikiwaaminisha wateja wake katikati mwa miaka ya ’90. Bahati mbaya, sasa imani hiyo imekuwa historia. Baada ya hapo Deutsche Bank imekuwa ikiichezea kamari imani hiyo ya wateja wake. 

Kwa kuwa taasisi hiyo ya kifedha ilitaka iwe na satwa kubwa kwenye ushindani, kanuni zote njema zikatupwa nje, maana walidhani kwamba isingeliweza kupata mafanikio kwa kuzifuata. Ili kutengeneza faida kubwa kwa kila muamala inaohusika nao, Deutsche Bank ikajigeuza kuwa mashine ya kutengeza fedha kwa namna yoyote iliyopo mbele yake.

Ama kwa kufanya ghiliba kwenye viwango cha riba, utakatishaji fedha, mikataba ya mikopo yenye usalama hafifu, au mahusiano ya kibiashara na wateja wenye rikodi ya kutia mashaka kama vile mtuhumiwa wa udhalilishaji watoto kingono, Jeffery Epstein, Benki hiyo ya Ujerumani ilikuwa na mkono wake kwenye kila mchezo, kila mahala. 

Boehme Henrik Kommentarbild App

Henrik Boehme

Yumkini ikiamini kuwa kila uchafu ukiwa mwingi, ndivyo faida navyo inavyoongezeka. Na kama majalada ya FinCEN yanavyoonesha, Deutsche Bank ipo kwenye orodha ya juu maana zaidi ya nusu ya ripoti za miamala inayoshukiwa inahusiana moja kwa moja na benki hiyo.

Uroho na ufisadi si njia sahihi

Msimamizi wa masuala ya fedha nchini Marekani alizungumzia kile anachokiita "uroho na ufisadi"  kwenye ripoti yake ya mwisho pale shughuli za utakatishaji fedha nchini Urusi zilipoibuliwa mnamo mwaka 2015. Deutsche Bank ilikuwemo pia kwenye kashfa hiyo.

Leo tena inaonekana kuwa bado uroho na ufisadi umo kwenye mfumo wa Deutsche Bank. Baada ya kupigwa faini ya dola milioni 600, benki hiyo iliahidi kujisafisha. Kwa hakika, tangu hapo benki hiyo ya makao yake makuu mjini Frankfurt imewekeza takribani dola bilioni moja katika kuimarisha mifumo yake ya udhibiti na kuongeza watu 1,500 kwenye idara inayohusika na udhibiti huo. 

Lakini ugunduzi huu wa sasa unaonesha kwamba mikataba hii ya kifisadi ya Urusi ilikuwa ikiendelea hata baada ya hapo. Mwaka 2017, kwa mfano, benki hiyo ilituma miamala yenye mashaka kwa mamlaka za Marekani juu ya biashara zilizoko Urusi.

Kama ilivyotegemewa, Deutsche Bank inakanusha tuhuma zote dhidi yake. Kwanza, inasema yenyewe ilishaorodhesha michakato yote iliyowekwa hadharani na majalada ya FinCEN na, pili, yote hayo yaliyotokea kwenye kipindi kinachoishia mwaka 2016. Na sasa hii ni "benki nyengine". Pia tuhuma dhidi ya mkuu wa benki hiyo, Christian Sewing, hayana msingi, maana yeye alishika nafasi hiyo mwaka 2018. Ndivyo inavyodai Deutsche Bank.

Lakini ukweli ni kuwa Sewing alikuwa mkuu wa ukaguzi wa ndani kwa miaka mitano kabla ya hapo na idara yake ndiyo iliyokuwa ikifuatilia biashara za Urusi na isigunduwe chochote. Sasa wanatwambia kuwa kamwe hakuwa kuona wala kusaini matokeo ya uchunguzi wowote.

Hakika hii ni hoja dhaifu kumchomowa mkuu wa sasa wa Deutsche Bank kwenye lawama.

Lakini hachomoki!
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com