Mandela atimiza miaka 95 ya kuzaliwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mandela atimiza miaka 95 ya kuzaliwa

Rais wa zamani wa Afrika Kusini mzee Nelson Mandela leo (18.07.2013) ametimiza miaka 95, akiwa amelazwa hospitalini kwa muda wa wiki sita. Ikulu ya nchi hiyo imesema hali ya mkongwe huyo inaonyesha kuboreka kidogo.

Mandela atimiza miaka 95 hospitalini

Mandela atimiza miaka 95 hospitalini

Salamu zimemiminika leo kumpongeza mzee Nelson Mandela na kumtakia nafuu ya haraka. Rais Barack Obama wa Marekani amesema katika salamu zake kwamba yeye na familia yake walitiwa hamasa na ushujaa wa Mandela, baada ya kutembelea gereza alikofungiwa kwa miaka mingi wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Mapema leo Ikulu ya Afrika Kusini imetoa tangazo linaloarifu juu ya afya ya mzee Mandela. ''Madiba anabakia hospitalini mjini Pretoria, lakini madaktari wanaomtibu wanathibitisha kuwa hali yake inaboreka taratibu'', lilisema tangazo hilo, likitumia jina la kiukoo la Mandela..Madiba.

Mbali na kumpongeza Mandela kwa kutimiza miaka 95, Rais Obama ametoa wito kwa watu kuadhimisha siku ya Mandela wafanya kazi za kujitolea kwa kuenzi jina lake.

Mfano wa kuigwa

Mzee Mandela wakati akimsaidia rais Zuma katika kampeni yake ya urais

Mzee Mandela wakati akimsaidia rais Zuma katika kampeni yake ya urais

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amewataka watu kuiga mchango wa Mandela na kujitolea kwake, kwa kuongeza juhudi za kuiendeleza jamii yao. Zuma mwenyewe atawakilisha mtazamo wa Mandela wa kuzileta pamoja jamii, kwa kuwapa nyumba watu masikini weupe.

Katika juhudi hizo, waendesha baskeli watafanya usafi mitaani, wafanyakazi wa kujitolea watapaka shule rangi, na wanasiasa watashiriki katika miradi mingine ya kujitolea kwa muda wa dakika 67, kutambua miaka 67 ambayo Mandela amekuwa mtumishi wa umma. Aidha, wanafunzi wataanza siku yao shuleni kwa kuimba wimbo '' Happy Birthday Mandela'' wakimtakia heri na kumpongeza kwa kutimiza umri huo wa miaka 95.

Shughuli nyingine itakayofanyika kuadhimisha miaka 95 ya Nelson Mandela, ni kumkabidhi mkongwe huyo kitambulisho kipya cha kisasa, ambacho kitapokelewa kwa niaba yake na bintiye Zindzi.

Kumbukumbu ya mapambano dhidi ya ubaguzi

Mandela anasifiwa kote duniani kwa kusimama kidete dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote

Mandela anasifiwa kote duniani kwa kusimama kidete dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote

Tukio hilo litakuwa na viashiria mbali mbali kama kumbu kumbu ya enzi za ubaguzi wa rangi, ambapo raia weusi walilazimishwa kubeba vitambulisho, na hawakuruhusiwa kutembea katika baadhi ya maeneo, kwa baadhi ya nyakati.

Mwaka 2010, Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 18 Julai kuwa siku ya Mandela, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel ya Amani, lakini mwaka huu, siku hii imekuwa na umuhimu mkubwa zaidi.

Mandela amalazwa hospitalini kwa siku 41 sasa akiugua maambukizi ya mapafu, na kwa muda mrefu hali yake imetajwa kuwa mbaya, lakini ambayo imedhibitiwa na madaktari.

Watu wa familia yake wamesema kuwa hali hiyo imeimarika kwa kiasi fulani, na anaweza kupumua kwa msaada wa mashine. Binti yake Zindzi jana aliliambia shirika la habari la Sky News kwamba kuna wakati walipokuwa wamekata tamaa wakijiweka tayari kupokea habari mbaya, na kuongeza kuwa kwa sasa anawapa matumaini.

Watu mbali mbali mashuhuri na wa kawaida wameahidi kujiunga na wananchi wa Afrika Kusini leo, kumuunga mkono Mzee Mandela katika siku kuu yake ya kuzaliwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE

Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com