Mali yajadiliwa Yamoussoukro | Matukio ya Afrika | DW | 27.02.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mali yajadiliwa Yamoussoukro

Viongozi wa jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, wanakutana Yamoussoukro nchini Côte d'Ivoire kuzungumzia vita nchini Mali na namna ya kushika nafasi itakayoachwa na wanajeshi wa Ufaransa

Viongozi wa jumuia ya ECOWAS katika mkutano wao wa kilele mjini Yamoussoukro

Viongozi wa jumuia ya ECOWAS katika mkutano wao wa kilele mjini Yamoussoukro

Mkutano huu wa kilele unafanyika siku moja baada ya shambulio jengine la kigaidi lililoangamiza maisha ya watu kadhaa huko Kidal, mji wa ncha ya mbali ya kaskazini mashariki ya Mali wanakokutikana wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Chad. Shambulio hilo linatoa picha halisi ya hali namna ilivyo nchini Mali.

Viongozi wa mataifa 15 wanachama wa jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika magharibi, ECOWAS, wanakutana katika mji mkuu wa Côte d'Ivoire,Yamoussoukro, kujaribu kuharakisha juhudi za kutumwa kikosi cha wanajeshi wa kiafrika wanaoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, AFISMA, nchini Mali.

Kutokana na "vita visivyo vya kawaida" vinavyoendeshwa na makundi ya wanamgambo wa kiislamu,Côte d'Ivoire ambayo ndio mwenyekiti wa jumuiya ya ECOWAS, imetoa wito wa msaada ziada wa fedha kugharimia shughuli za kikosi cha AFISMA.

Katika wakati ambapo jumuiya ya kimataifa imeahidi mwishoni mwa mwezi uliopita kuchangia Euro milioni 338 kwa ajili ya kikosi cha AFISMA, jeshi la Mali na huduma za kiutu, Cote d'Ivoire inasema gharama jumla zimeongezeka maradufu na kufikia Euro milioni 715.

Duru za kuamainika zinasema jumuia ya ECOWAS inapanga kutuma wanajeshi 2000 zaidi ya 6000 walioahidi.

Hakuna haja ya Pupa

Mali Konflikt

Wanajeshi wa Guinea katika kikosi cha Afrika nchini Mali

Kishindo ni kikubwa kikosi hicho cha Afrika kinalazimika kushika nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa waliofanikiwa kwa ushirikiano pamaoja na wanajeshi wa Mali kuwatimuwa wanamgambo wa kiislam toka miji mikuu ya kaskazini ya Mali.

Lakini wadadisi wengi wanaahisi wanajeshi wa Mali na wale wa AFISMA hawana uwezo kwa sasa wa kulidhibiti peke yao eneo lote la kaskazini ya Mali.

Ufaransa yenye wanajeshi elfu nne nchini humo,na ambayo imeelezea azma ya kujitenga kuanzia mwezi ujao imeanza kubadilisha msimamo wake."Hakuna haja ya kuondoka kwa pupa.Kila kitu kitatendeka kwa mpango " hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa kabla ya mazungumzo kati ya rais Francois Hollande na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry mjini Paris.

Wakati wa mkutano huo wa Yamussukro unaotarajiwa kumalizika kesho, viongozi wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi wanatazamiwa kumchagua tena rais Alassane Ouattara wa Côte d'Ivoire aendelee kuwa mwenyekiti wa jumuia hiyo kwa mhula mwengine wa mwaka mmoja.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri Josephat Charo

DW inapendekeza