1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yaishtumu Ufaransa kwa kuipeleleza

Admin.WagnerD27 Aprili 2022

Utawala wa kijeshi Mali umeishtumu Ufaransa kwa kukiuka mara kwa mara anga linalodhibitiwa katikati na kaskazini mwa nchi hiyo ili kuvipeleleza vikosi vyake, katika ongezeko la karibuni la mzozo kati ya Paris na Bamako.

https://p.dw.com/p/4AWLq
Mali Takuba Franzosen in Menaka Militär-Camp
Picha: THOMAS COEX/AFP/Getty Images

Katika taarifa iliyotolewa jana jioni,serikali ya kijeshi ya Mali ilisema matukio zaidi ya 50 ya ukiukaji wa anga la taifa hilo yamerikodiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu, hasa yakifanywa na ndege za Ufaransa.

Uhusiano mbaya kati ya Ufaransa na utawala wa kijeshi katika koloni lake hilo la zamani umeisukuma kuondoa wanajeshi wake waliokuwa wamepelekwa huko tangu mwaka 2013 kupambana dhidi ya wanagambo wenye mafungamano na mitandao ya Al-Qaeda na Dola la Kiislamu.

Mali Französische Soldaten
Wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa kwenye kambi ya Gossi.Picha: Daphné Benoit/AFP/Getty Images

Taarifa ya serikali ya Mali imetaja tukio mojawapo la karibuni zaidi la ukiukaji wa anga lake kuwa urushaji haramu wa ndege isiyotumia rubani Aprili 20 juu ya kambi ya kijeshi ya Gossi kaskazini mwa Mali, siku moja bada ya Ufaransa kuikabidhi kambi hiyo kwa Mali kama sehemu ya mchakato unaoendelea wa kuondoa majeshi yake.

Soma pia: Mali yaituhumu Ufaransa kuchafua sifa ya jeshi lake

Taarifa hiyo iliongeza kuwa ndege za Ufaransa kisha ziliruka na kurudi juu ya msafara wa wanajeshi wa Mali waliokuwa wanaelekea Gossi Aprili 21.

Shutuma hizo zinafuatia mchezo wa kulaumiana wa wiki iliyopita kuhusu picha zilizopigwa na ndege zisizo na rubani zilizoonesha wanajeshi karibu na kambi ya Gossi wakiwa wamefunika maiti kwa mchanga, zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku mtumiaji mmoja wa Twitter aliejitambulisha kama afisa mstaafu wa Mali akiwashutumu wanajeshi wa Ufaransa.

Soma pia: Mali yampa balozi wa Ufaransa saa 72 kuondoka nchini humo

Ufaransa ilijibu shutuma hizo kwa kusema kwamba ilikuwa inatengenezewa mizengwe, huku jeshi likisema wanaume walioonekana kwenye mkanda wa video walikuwa mamluki wa Urusi wanaotuhumiwa kulisaidia jeshi la Mali kupambana dhidi ya wanamgambo na kuuawa raia katika operesheni zao.

Mali | Übergangspräsident Assimi Goïta
Kiongozi wa mpito wa Mali Assimi Goita.Picha: Präsidentschaft der Republik Mali

Lakini jeshi la Mali lilisema wiki iliyopita kwamba wanajeshi wake waligundua kaburi la halaiki karibu na Gossi baada ya kuchukua udhibiti wa kambi hiyo, na kwamba kiwango cha uozo wa miili hiyo kilionyesha kuwa mauaji yalikuwa yametokea mapema zaidi.

Soma pia:Umoja wa Mataifa wataka kuchunguza mauwaji ya Mali

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa haikupatikana mara moja kuzungumzia tuhuma hizo.

Uamuzi wa Ufaransa kuondoa wanajeshi wake nchini Mali ulikuja baada ya uhusiano na jeshi lililotwaa madaraka mwaka 2020 kuzorota pakubwa. Suala moja kuu limekuwa ushirikiano wa Mali na wapiganaji kutoka kundi la Urusi la Wagner.

Lakini Mali na Urusi zinasema ni wakufunzi tu wa kijeshi wa Urusi ndiyo walioko nchini humo, na ikulu ya Kremlin inakusha kuwa na uhusiano na kundi la Wagner.