Makubaliano yashindikana tena kupatikana nchini Yermen | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Makubaliano yashindikana tena kupatikana nchini Yermen

Rais wa Yemen akataa kwa mara nyengine tena kutia saini makubaliano ya kipindi cha mpito kumaliza miezi minne ya malalamiko ya umma. Marekani imevunjika moyo na jambo hilo.

default

Maandamano dhidi ya serikali ya Yemen mjini Sanaa

Rais Ali Abdullah Saleh, ambae maelfu ya waandamanaji wanapaza sauti tangu januari mwaka huu kumtaka ang'atuke baada ya miaka zaidi ya 30 madarakani, anahoji makubaliano yaliyofikiwa yanaweza kuitumbukiza Yemen katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ameutwika jukumu la hali hiyo upande wa upinzani ambao umetia saini makubaliano hayo tangu jumamosi iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba limeamua kusitisha juhudi zake za upatanishi, huku waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton, akilalamika na kusema tunanukuu:"Rais Saleh ndie pekee anaekataa kutekeleza kivitendo matamshi aliyoyatoa." Mwisho wa kumnukuu.

Katibu mkuu wa baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba, Abdullatif al-Zayani, ameshaondoka Sanaa baada ya rais Ali Abdullah Saleh kutoa masharti mepya akiutaka upande wa upinzani utie saini makubaliano hayo mbele yake, na katika kasri lake.

USA China Treffen in Peking Flash-Galerie

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton

"Marekani imevunjika moyo kutokana na rais Saleh kukataa kwa mara nyengine tena kutia saini makubaliano ya kung'oka madarakani ." Amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, bibi Hillary Clinton.

Rais Ali Abdullah Saleh ameshawahi mara mbili hapo kabla kukataa kutia saini makubaliano ya kipindi cha mpito yanayotaja rais aondoke madarakani siku 30 baada ya kutia saini makubaliano hayo na badala yake apatiwe kinga yeye na wapamabe wake ya kutoandamwa kisheria.

Auseinandersetzung zwischen Polizei und Demonstranten Yemen

Polisi wapambana na waandamanaji mjini Sanaa

Upande wa upinzani unaihimiza Marekani na Saud Arabia wazidi kumshinikiza rais Saleh. Wameahidi maandamano yataendelea mpaka rais Saleh anang'oka madarakani.

Watu waliokuwa na silaha waliuzingira ubalozi wa falme za nchi za kiarabu- nchi mojawapo mwanachama wa baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba. Waliwazuwia wanadiplomasia wasiende kuonana na rais Ali Abdullah Saleh.

Maelfu ya wapinzani wa rais ali Abdullah saleh waliteremka majiani mjini Sanaa jana kwa kile kinachoangaliwa kama maandamano makubwa kabisa kuwahi kufanyika tangu malalamiko ya umma yalipoanza januari mwaka huu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/reuters,afp

Mhariri:Miraji Othman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com