1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahamat Deby, rais mpya wa Chad

21 Aprili 2021

Raia wa kawaida humuita Mahamat 'Kaka', yaani Mahamat wa Bibi kwa kuwa amelelewa na bibi yake mzaa baba, na wanajeshi wenziwe humuita "miwani myeusi" kwa kuwa anapendelea kuvaa miwani ya giza. Sasa ndiye rais wao.

https://p.dw.com/p/3sJ2Y
Tschad Mahamat Idriss Déby Itno
Picha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Mara tu baada ya kutangazwa kifo cha baba yake aliyeitawala Chad kwa miongo mitatu ya mkono wa chuma, Mahamat, mwenye umri wa miaka 37, alipanda cheo ghafla na kuwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo ya jangwa. 

Hadi masaa machache kabla ya kutangazwa, kwa wengi jenerali huyu mvaa miwani myeusi mwenye nyota nne begani alikuwa kijana tu aliyepewa jukumu la kusimamia kikosi maalum cha ulinzi wa baba yake, kiitwacho DGSSIE, na hakuwemo kabisa kwenye orodha ya warithi wa Rais Deby. 

Kama kulikuwa na mtu wa karibu kifamilia kutajwa, basi angelikuwa kaka yake, Abderahman, ambaye ni naibu mkurugenzi wa ofisi ya rais.

Lakini badala yake ni Mahamat aliyechukuwa madaraka na haraka kuwateuwa majenerali 14 kuunda serikali itakayoitawala Chad hadi "uchaguzi huru na wa kidemokrasia" ndani ya kipindi cha miezi 18.

Kama baba yake, Mahamat ni mwanajeshi kitaaluma na kikazi

Tschadische Soldaten bei Rückkehr aus Mali 13.05.2013 mit Präsident Idriss Deby Itno
Katika picha hii ya tarehe 13 Mei 2013, marehemu Rais Idriss Deby (katikati) akiinuwa mikono ya mkuu wa kikosi cha Chad nchini Mali, Jenerali Oumar Bikimo (kushoto) na naibu wake, Mahamat Idriss Deby (kulia).Picha: STR/AFP/Getty Images

Mahamat alipata mafunzo ya kijeshi muda mfupi nchini Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Chad, na kisha kuendelea na mafunzo nchini mwake kabla ya kujiunga na kikosi maalum cha rais, ambako nako alipanda ngazi haraka haraka hadi akawa mkuu wa kikosi hicho. 

Mwaka 2009 alipata sifa kubwa baada ya ushindi dhidi ya wanajeshi walioasi wakiongozwa na binami yake aitwaye Timan Erdimi, wakitokea mashariki na waliokaribia kuichukuwa ikulu mjini N'Djamena kama si uingiliaji kati wa wanajeshi wa Ufaransa.

Mwaka 2013 alipewa jukumu la kuwa naibu mkuu wa kikosi cha nchi yake nchini Mali, kulikomuweka karibu na wanajeshi wa Kifaransa wanaopambana na makundi ya itikadi kali.  

Mahamat wa Bibi

Tschad Mahamat Idriss Déby Itno
Rais mpya wa Chad, Mahamat Idriss Deby, akiwa kwenye kituo cha kupigia kura tarehe 11 Aprili 2021. Baba yake alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo siku hiyo hiyo aliyotangazwa kifo chake tarehe 20 Aprili 2021, naye kutawazwa kuwa rais.Picha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Wachad wengi wanamfahamu tu kwa jina la Mahamat "Kaka", yaani "Mahamat wa Bibi" kwa Kiarabu cha Chad, kutokana na kulelewa na bibi yake mzaa baba.

Kwa wanajeshi wengi, humuita "ttu mwenye miwani myeusi", anayesemekana kuwa msiri, mpole lakini mwenye kuwahurumia walio chini yake. 

Kama baba yake, Mahamat anatokea kabila la Zaghawa ambalo limekuwa likitowa maafisa wengi wa kijeshi, lakini katika siku za karibuni kumekuwa na mpasuko ndani ya kabila hilo uliomfanya Rais Deby kuwahamisha maafisa kadhaa wa kijeshi. 

Mama yake Mahamat anatokea kabila jengine la Sharan Goran kama alivyo mke wake, Dahabaye Oumar Souny, mwandishi wa habari wa rais na binti wa mshirika wa rais wa zamani, Hissene Habre, aliyepinduliwa na Idriss Deby mwaka 1990.

Wataalamu wanasema hii ni sababu mojawapo ya jamii ya Zaghawa kumuangalia Mahamat kwa mashaka, na huenda kukawa na kipindi cha kuwekana sawa.