1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magonjwa  yahofiwa kuwakumba  waathiriwa wa Idai Msumbiji

25 Machi 2019

Magonjwa ya mlipuko, yanahofiwa kuwakumba  waathiriwa wa kimbunga Idai nchini Msumbiji na baadhi ya nchi za Kusini mwa bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/3Fcbo
Mosambik Zyklon Idai | Zerstörung und Hilfe
Picha: Reuters/S. Sibeko

 Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa masuala ya kiutu, pamoja na serikali ya Msumbiji magonjwa ya mlipuko huenda yakasababisha matatizo makubwa.

Akizungumza mjini Beira Waziri wa ardhi wa Msumbiji Celso Correia amesema ni wazi lipo tishio la magonjwa kama vile Malaria na kipindupindu. Waziri Correia amewaomba raia wa nchi hiyo wasiogope na kwamba pamoja na kitisho hicho tayari serikali inatengeneza mazingira ya kutoa tiba na kuzuia kusambaa kwa magonjwa ya kipindupindu. Correia amesema, kitisho cha Malaria kinatokana na mazingira yaliyopo hivi sasa kwani maeneo mengi yamejaa maji, hivyo ni hakika kwamba raia wanakabiliwa na hatari ya ugonjwa huo.

Waathiriwa wa kimbunga Idai bado wako katika wakati mgumu, wengi wao wakiwa bado wanaishi katika mapaa ya nyumba, huku wale ambao tayari wamekwisha kuokolewa wakiwa wanauhutaji mkubwa wa chakula na dawa. Kwa mujibu wa mamlaka ya uratibu wa masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa OCHA takribani wanawake 74,600 walioathiriwa na kimbunga hicho ni wajawazito na asilimia sitini kati yao wanatarajiwa kujifungua ndani ya miezi sita ijayo.

Mosambik Cholera Idai Zyklon
Mashua za uvuvi zikishiriki katika uokoaji nchini huko Buzi, MsumbijiPicha: picture-alliance/dpa/K. Bartlett

Familia zawatafuta  waliopotea

Wakati huohuo, maelfu ya familia katikati ya nchi hiyo wameendelea kuwatafuta ndugu zao waliotoweka baada ya kimbunga idai kilichofuatiwa na mafuriko. Juhudi za kuwaokoa watu bado zinaendelea ambapo mashua za wavuvi  zimeonekana zikisaidia zoezi la uokoaji  kati ya eneo la Buzi na mji wa Bandari wa Beira ulioathiriwa vibaya na mafuriko yaliotokea baada ya kimbunga. Akizungumzia madhara ya kimbunga hicho mmoja wa watu walionusurika na kimbunga hicho Domingo Muchanga amenukuliwa akisema, ''Mabati mawili yameezuliwa na upepo. Hayo mabati sijui nitayanunua vipi tena. Hii nyumba nilijenga muda mrefu uliopita na ilikuwa nafuu sana lakini sasa ujenzi ni ghali mno.''

Kimbunga  Idai kiliikumba Msumbiji Machi 14, karibu na mji wa bandari wa Beira nakusababisha upepo mkali ulioambatana na mafuriko. Kutokana na mafuriko, mito mikubwa miwili Buzi na Pungue ilizidiwa na maji na kupasuka kisha kuvizamisha vijiji vya eneo hilo huku miili ya watu ikielea. Idadi ya watu waliokufa kutokana na kimbunga hicho imefikia 446 kwa Msumbiji, 259 nchini Zimbabwe na Takribani 56 huko Malawi na kuifanya idadi ya waliokufa kutokana na janga hilo kufikia 761 katika nchi hizo tatu za kusini mwa bara la Afrika.

Mwandishi Angela Mdungu/AFP/APE

Mhariri: Sekione Kitojo