1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya ng'ombe wapigwa mnada kaskazini mwa Tanzania

Veronica Natalis
16 Desemba 2022

Ng'ombe 1700 kutoka kaya 27 za jamii ya wafugaji ya Maasai wakazi wa Loliondo mkoani Arusha kaskazini mwa Tanzania, wamepigwa mnada kwa amri ya mahakama kutokana na kuingia katika eneo la hifadhi ya taifa ya Serengeti

https://p.dw.com/p/4L2tW
Landwirte Tierlandwirtschaft Herde Kühe Bauern Landwirte Farmer
Picha: Getty Images/T. Karumba

Hatua hiyo inaendelea kuleta ugumu wa maisha kwa jamii hiyo kwani kwa sasa pia idadi kubwa ya mifugo inakufa kutokana na ukame unaoyakumba maeneo mengi. 

Mahakama ya wilaya ya Serengeti Mkoani Mara kaskazini mashariki mwa Tanzania, ilitoa amri ya kuuzwa kwa mifugo hao  kwa mujibu wa sheria inayohusu mali isiyo na mwenyewe ya mwaka 1958 inayozuia mifugo kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kama hifadhi hiyo ya taifa ya Serengeti inayotajwa kuwa hifadhi bora duniani.  Amri hiyo ya mahakama ilibainisha kwamba mifugo hao hawakuwa na wenyewe au waliokotwa hifadhini,  jambo ambalo linakanushwa vikali na baadhi ya watu kutoka jamii hiyo. 

Ng'ombe hao wanaelezwa kukamatwa na kutaifishwa kwa awamu nne, huku mawakili upande wa utetezi wakibainisha kwamba wamiliki wa Ng'ombe hao waliogopa kujitokeza kwa kuhofia kukamatwa, kufuatia hali ilivyo kwa sasa eneo la Loliondo baada ya baadhi ya wakazi na viongozi kufunguliwa mashitaka mbali mbali na wengine kufuatiliwa.

Pamoja na mambo mengine mawakili wanashauri kwamba wamiliki wa ng'ombe waendelee kujengewa uwezo wa masuala ya kisheria, na serikali itafute njia nzuri ya kushughulikia suala la mifugo inayovuka mipaka hasa katika kipindi hiki cha ukame ambapo malisho na maji ya mifugo ni adimu. 

Katika maeneo mengi ya jamii ya wafugani ya Maasai hasa katika wilaya za Ngorongoro, Monduli na Longido, idadi ya mifugo wanaokufa kwa kukosa malisho na maji inaendelea kuripotiwa huku suala hilo likihusishwa na ukame unaondelea kuyakumba maeneo hayo. 

Veronica Natalis: DW Arusha