1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakimbia mashambulizi kaskazini mwa Msumbiji

John Juma
28 Februari 2024

Serikali ya Msumbiji imethibitisha kuwa maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makaazi yao kutoka eneo linalokumbwa na machafuko kaskazini mwa taifa hilo kufuatia wimbi la mashambulizi ya wanamgambo wa itikadi kali.

https://p.dw.com/p/4czcy
Cabo Delgado, Msumbiji
Polisi wa Msumbiji wakifanya doria katika mji wa kaskazini, Cabo Delgado mwezi Agosti 2023.Picha: Delfim Anacleto

Hata hivyo, serikali hiyo ilikanusha miito ya hali ya hatari.

Akizungumza na waandishi habari na kuelezea hali ilivyo katika mkoa wa Cabo Delgado, msemaji wa serikali, Filimao Suaze, alisema takribani watu 67,321 wameyakimbia makaazi yao.

Soma zaidi: Msumbiji: Raia sita wauawa kwa kukatwa vichwa na mtawa mmoja auawa kwa kupigwa risasi kichwani

Kwa mujibu wa ripoti za ndani na takwimu za Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM), machafuko mapyayalizuka kaskazini mwa Msumbiji wiki mbili zilizopita,

IOM imesema zaidi ya watu 71,681 walikimbia machafuko kati ya Disemba 22 na Februari 25.

Kati ya Jumatano na Alhamisi wiki iliyopita, zaidi ya wakimbizi wapya 30,000 walisajiliwa kuwasili mji wa Namapa kwa mabasi, boti au kwa kutembea.