1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu wakadiriwa kufa nchini Haiti

13 Januari 2010

Ni baada ya kutokea janga la tetemeko kubwa la ardhi

https://p.dw.com/p/LUig
Baadhi ya wakaazi wa jiji la Port-au-Prince wakijaribu kutafuta jamaa zao walionasa katika vifusi, kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea jana.Picha: AP

Maelfu ya watu wanakadiriwa kufa nchini Haiti baada ya kutokea tetemeko kubwa la ardhi lililokikumba kisiwa hicho hapo jana.

Tetemeko hilo kubwa lilitokea kilomita 15 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo na kuharibu majengo mengi ya jiji hilo, ikiwemo Ikulu ya rais.

Tetemeko hilo linaelezwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea katika kisiwa hicho katika kipindi cha karne mbili zilizopita.

Baadhi tu ya majengo yaliyoharibiwa vibaya na tetemeko hilo ni Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa visiwani humo, Ikulu ya rais pamoja na hoteli kadhaa zilizokuwa zimefurika watalii wengi kutoka nchi za magharibi.

Picha za televisheni zilionesha watu walionusurika wakijaribu kujitoa katika vifusi vizito.

Haiti ni nchi maskini zaidi katika eneo la upande wa magharibi wa dunia, na hivyo kusababisha harakati za uokoaji kuwa ngumu zaidi kutokana na mifumo duni ya miundombinu.

Mitandao ya simu imeripotiwa kukatika, huku moto mkubwa ukishuhudiwa katikati ya jiji la Port-au-Prince, moto ambao umesababishwa na kupasuka kwa mabomba ya gesi.

Mara tu baada ya tetemeko hilo, mashuhuda wanasema walisikia kishindo kizito kilichofuatiwa na mwanga mkali uliotanda mitaa ya Port-au-Prince, na vumbi jingi lilitapakaa katika anga ya jiji hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amelitaja tetemeko hilo kama janga kubwa la karne.

Huku jiji hilo likiwa katika kiza kikubwa, idadi ya vifo na kiwango cha madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo ni vigumu kukadiria.

Uwanja wa ndege wa jiji hilo pia umeripotiwa kuharibika kabisa, na mashirika ya misaada ya kiutu yanajiuliza njia itakayotumika kufikisha misaada katika eneo hilo pamoja na vikosi vya uokoaji.

Ufaransa, iliyokuwa koloni kubwa katika kisiwa hicho, imetangaza leo kupeleka mara moja ndege mbili za misaada pamoja na wafanyakazi 60 wa uokozi.

Canada pamoja na baadhi ya mataifa ya Amerika ya Kusini pia yametangaza kushiriki katika juhudi za uokoaji.

Ikulu ya Marekani imesema serikali ya Rais Barack Obama wa nchi hiyo imesimama imara kuwasaidia watu wa Haiti.

Mjini Miami vikosi vya uokoaji vya majini vimeziweka tayari mashua zake kwa kutoa misaada yoyote itakayohitajika kwa njia ya maji.

Nchini Uingereza, msemaji wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa amesema nchi hiyo inalichukulia janga la tetemeko hilo kwa uzito mkubwa na kikosi chake cha kutathimini majanga kipo tayari kuelekea nchini Haiti hii leo.

Nalo Shirika la Misaada la Kimataifa la Uingereza, Oxfam, limesema tayari vikosi vyake ya utoaji misaada vimewasili katika eneo hilo, vikiwa na shehena ya misaada ya kiafya na maji.

Wakati huo huo, kilomita 80 kutoka Haiti kunapatikana mji wa Baracoa uliopo nchini Cuba, ambapo wakaazi wa mji huo iliopo kwenye pwani ya mashariki wameondolewa ikiwa ni hatua ya tahadhari, baada ya tetemeko hilo kuashiria dalili ya kimbunga cha Tsunami.

Tetemeko lililotokea nchini Haiti lilisikika pia nchini Cuba.

Mwandishi:Lazaro Matalange/AFP/DPA/RTRE

Mhariri:Othman Miraji