Maelfu waandamana Kyrgyzstan huku matokeo ya bunge yakifutwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.10.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maelfu waandamana Kyrgyzstan huku matokeo ya bunge yakifutwa

Tume ya uchaguzi ya Kyrgyzstan imefuta matokeo ya uchaguzi wa bunge uliofanyika Oktoba nne wakati ambapo maelfu ya waandamanaji wakiyapinga matokeo hayo kwa kuvamia majengo ya serikali, na kumtorosha jela rais wa zamani

Mkuu wa tume ya uchaguzi Nurzhan Shaildabekova  amelieleza shirika la habari la Interfax kwamba uamuzi wa kufuta matokeo umechukuliwa ili "kuepuka mvutano" katika nchi hiyo.

Siku ya Jumatatu wafuasi wa upinzani nchini Kyrgyzstanwaliyavamia majengo kadhaa ya serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo Bishkek na kumtorosha rais wa zamani kutoka jela na kutangaza kwamba wana mipango ya kumuondoa madarakani rais na kuunda serikali mpya. Rais Sooronbai Jeenbekov amevishutumu "vikosi kadhaa vya kisiasa" kwa kujaribu "kunyakua mamlaka kinyume na sheria", katika taarifa aliyoitoa Jumanne na kuutaka upinzani kuwasihi watu kuondoka mitaani.

"Amani katika nchi na utulivu katika jamii ni muhimu zaidi kuliko mamlaka ya mwanasiasa yeyote. Ninapendekeza tume ya uchaguzi ichunguze kwa uhakika ukiukaji wowote wakati wa zoezi la uchaguzi na kufuta matokeo kama itahitajika. Ninawaomba viongozi wa vyama vya kisiasa kuwatuliza wapiga kura wao na kuwasihi kutoshiriki kwenye mikusanyiko yoyote", alisema rais huyo.

Maandamano makubwa katika mji mkuu wa Bishkek na miji mingineyo, yalizuka baada ya mamlaka kutangaza matokeo ya awali katika uchaguzi wa bunge uliofanyika Jumapili. Matokeo hayo yalivipatia ushindi vyama viwili vilivyo na ushirikiano na tabaka la utawala huku kukiwa na ripoti za ununuzi wa kura na ukiukwaji mwingine.

Wafuasi wa vyama kadhaa vya upinzani walimiminika mitaani siku ya Jumatatu, wakitaka kufutwa kwa matokeo hayo na kudai uchaguzi mpya. Polisi walitawanya umati wa waandamanaji kwa kutumia maji ya kuwasha, mabomu ya kutoa machozi na takribani watu 590 wamepata majeraha katika makabiliano na polisi na mtu mmoja kupoteza maisha kulingana na ripoti za shirika la habari la Interfax lililonukuu wizara ya afya ya Kyrgyzstan.

Waandamanaji walivamia eneo lenye majengo ya Bunge, ofisi ya rais pamoja na za jiji la Bishkek. Kundi jingine la waandamanaji lilielekea kwenye ofisi ya kamati ya taifa ya usalama, likidai kuachiwa kwa aliyekuwa rais wa zamani Almazbek Atambayev ambaye alihukumiwa kwa makosa ya ufisadi mapema mwaka huu na kupewa adhabu ya miaka 11 jela. Maafisa wa usalama walimuachia kiongozi huyo baada ya kufanya majadiliano na waandamanaji. Wafungwa wengine walioachiwa ni pamoja na mawaziri wakuu wawili wa zamani na wabunge wawili wa zamani.

Mgogoro huo ambao unakumbusha mapinduzi yaliyoshuhudia marais wawili wakiondolewa madarakani mwaka 2005 na 2010, utafuatiliwa kwa karibu na Urusi ambayo ina kambi ya kijeshi katika nchi hiyo isiyokuwa na bandari yenye wakaazi milioni 6.5 na iliyo jirani na China.