1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Machafuko mabaya yaikumba Haiti

Tatu Karema
6 Machi 2024

Taasisi ya mafunzo ya polisi katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince ilishambuliwa na genge la watu wenye silaha hapo jana Jumanne.

https://p.dw.com/p/4dDQU
Vikosi vya usalama vikishika doria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Port-au-Prince
Vikosi vya usalama vikishika doria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Port-au-PrincePicha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Ghasia hizo zinatokea wakati taifa hilo likitengwa zaidi kimataifa kufuatia shambulio kwenye uwanja wa ndege na kutoroka kwa wafungwa  jela.

Lionel Lazarre, afisa kutoka chama cha polisi cha Haiti, amesema shambulio dhidi ya taasisi hiyo, ambapo zaidi ya makuruta 800 wa polisi wanapata mafunzo, lilitibuliwa baada ya kuwasili kwa maafisa wa usalama wa ziada.

Soma pia: Kiongozi wa Haiti atua Puerto Rico akijaribu kurudi nyumbani 

Ghasia za hivi karibuni nchini humo, zimefuatia kuhamishwa kwa maelfu ya wakaazi kutoka mji huo mkuu huku Umoja wa Mataifa na Marekani zikielezea wasiwasi wao juu ya mzozo huo na magenge yenye silaha yakitangaza shambulio lililoratibiwa la kumtimua waziri mkuu wa nchi hiyo Ariel Henry.

Magenge hayo yanasema yanataka kuipindua serikali ya Henry, aliyekuwa nchini Kenya wikendi iliyopita kushinikza kupelekwa haraka kwa ujumbe wa polisi wa kimataifa unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kusaidia kuleta utulivu nchini mwake.