1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona yakwamisha maandamano ya siku ya wafanyakazi

Josephat Charo
1 Mei 2020

Wafanyakazi kote ulimwenguni wamelazimika kupunguza maandamano ya siku ya wafanyakazi leo kutokana na hatua zilizochukuliwa za kupiga marufuku mikusanyiko kwa lengo la kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3bePu
Deutschland Tag der Arbeit
Picha: Imago/IPON

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 70 siku ya wafanyakazi inaadhimishwa leo bila maandamano makubwa, huku matukio yakifutwa katika miji mikubwa ya Ujerumani kutokana na janga la virusi vya corona. Waandaaji wa maandamano hayo hapa nchini, kama vile Muungano wa vyama vya wafanyakazi na chama cha Social Democratic, SPD, wameandaa matukio katika mtandao wa intaneti.

Polisi wapatao 5,000 wanashika doria katika mji mkuu Berlin na wako katika hali ya tahadhari kuitawanya mikusanyiko inayovunja sheria ya watu kutojongeleana. Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Berlin Andreas Geisel ameiambia redio mjini humo kwamba polisi wanatakiwa wachukue hatua haraka, akionya kushiriki maandamano ambayo hayajaruhusiwa ni uhalifu. Zaidi ya maandamano 20 madogo yameidhinishwa mjini humo, watu wasiozidi 20 wakiruhusiwa kushiriki, tofauti kabisa na ilivyozoeleka ya maalfu kwa maalfu ya watu ambao hujitokeza mabarabarani kuandamana.

Huku Ufaransa ikikabiliwa bado na amri ya kufungwa shughuli za kawaida na mikusanyiko ya watu, wafanyakazi wanaiadhmisha siku yao katika mitandao ya kijamii au wakiwa katika roshani za nyumba zao. Phillipe Martinez, katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi Ufaransa, amesema hii ni fursa ya kuwajibika ili kuyatimiza matakwa ya jamii ambayo wamekuwa wakiyapigania kwa muda mrefu ambayo yamewekwa bayana na janga la corona.

Papa awaombea wafanyakazi

Katika makao makuu ya kanisa Katoliki, Vatican, kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Francis mapema leo kabla kuanza misa ya kila siku amewaombea wafanyakazi wote duniani. "Leo tunajiunga na wanaume na wanawake, waumi na wasio waumini, kuadhimisha siku ya wafanyakazi. Tunawaombea wanaopambana kupata haki kazini kwao, wafanyabiashara wazuri wanaofanya kazi zao kwa haki hata wanapopata hasara."

Vatikan | Papst Franziskus während Ostermesse im Petersdom
Papa FrancisPicha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Papa Francis alisema miezi miwili iliyopita alizungumza kwa njia ya simu na mfanyabiashara mmoja nchini Italia aliyemtaka amuombee kwa sababu hakutaka kumfuta kazi mtu yeyote. "Aliniambia: Kwa sababu kumfuta kazi mtu ni kujifuta mwenyewe. Fikra hii ni nzuri ya wafanyabiashara wengi wanaowalinda wafanyakazi wao kana kwamba ni watoto wao. Tuwaombee pia," aliongeza kusema.

Serikali ya Ugiriki imevitaka vyama vya wafanyakazi viahirishe mikutano ya hadhara na maandamano kwa zaidi ya wiki moja. Hata hivyo chama kikubwa cha wafanyakazi nchini humo kimeitisha mgomo kufanyika sambamba na siku ya wafanyakazi leo, na kimewataka waandamanaji wainue viganya vyao kuwapongeza wafanyakazi wa afya na wengine wanaosaidia kuhakikisha mahitaji na mawasiliano yanaendelea kuwepo.

Huko nchini Ureno muungano mkuu wa vyama vya wafanyakazi unapanga mkutano mkubwa wa viongozi katika eneo ambalo kwa kawaida hufanyika mkutano mkubwa wa hadhara kila mwaka.

Nchini Finland ambako maandamano makubwa hufanyika baada ya watu kukusanyika pamoja kula chakula katika mkusanyiko mkubwa kabisa wa watu wa mwaka, ni watu wachache tu waliokusanyika kuizunguka sanamu ya Manta katika uwanja mkubwa wa soko. Maafisa wa Finnland wameshauri siku ya wafanyakazi isherehekewe mtandaoni.

Huko Hong Kong waandamanaji wanaopigania demokrasia wanapanga kufanya maandamano baadaye leo, wakikaidi zuio la mikusanyiko wakati huu wa janga la corona, huku ghadhabu kuelekea China ikiibuka tena upya. Vyama vya wafanyakazi vinavyounga mkono demokraisa na miito iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii imewataka watu wapaze sauti katika vitongoji wanamoishi leo mchana, licha ya marufuku ya mikusanyiko wa watu wanne katika maeneo ya umma inayonuiwa kuepusha kuenea kwa virusi vya corona.

(afpe/dpae)