Maandamano Ulaya:Euro iko salama? | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 25.02.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Maandamano Ulaya:Euro iko salama?

Nchini Ugiriki,mgomo unaendelea kote nchini humo ulioukwamisha usafiri wa ndege na barabara.Maelfu ya abiria wamekwama katika vituo vya usafiri kwasababu ya mgomo huo utakaodumu kwa kipindi cha saa 24.

default

Waandamanaji mjini Athens


Wafanyakazi wa umma na makampuni ya binafsi wamegoma ili kuzipinga hatua zilizochukuliwa na serikali za kuipunguza nakisi ya bajeti..Huu ni mgomo wa pili kufanyika nchini humo kwasababu ya hatua hizo.Mgomo huu unafanyika wakati ambapo mataifa mengine ya Uhispania na Italia yanakabiliwa na matatizo ya fedha.

Kiasi cha zaidi ya wafanyakazi milioni 3 wa umma na makampuni binafsi wanashiriki katika mgomo huo wa utakaodumu kwa kipindi cha saa 24.Wafanyakazi hao wamechukua hatua hiyo baada ya serikali ya Ugiriki kuuongeza umri wa kustaafu,kubana matumzi ya sekta ya umma pamoja na kuzuwia nyongeza za mishahara kwa minajili ya kuipunguza nakisi ya bajeti yake.

Nakisi ya bajeti

Serikali ya Ugiriki inalazimika kuipunguza nakisi ya bajeti kutokea asilimia 12.7 hadi 3 ifikapo mwaka 2012 kama unavyodai Umoja wa Ulaya.Kwa sasa Ugiriki sharti ipunguze nakisi hiyo kwa asilimia 4 ifikapo mwaka ujao.Maria Kapelaki ni mfanyakazi katika sekta ya uuma na anayaunga mkono maandamano hayo,na '' Bila shaka nitashiriki kwenye mgomo huu..lazima tujitetee.Serikali ina madeni makubwa kwasababu ya mabenki.Kwani ninapaswa kuyalipa?La hasha!''alisisitiza.

Umoja wa Ulaya umelazimika kuishinikiza Ugiriki kuchukua hatua za kuipunguza nakisi ya bajeti yake kwasababu ya hofu kuwa sarafu ya euro huenda ikaathirika.Sarafu ya euro inatumiwa na mataifa 16 barani Ulaya.

GREECE_PROTEST32.jpg

Polisi wa kuzuwia ghasia Ugiriki

Kubana matumizi

Ili kulitimiza hilo serikali ya Ugiriki imelazimika kuzuwia nyongeza zote za mshahara katika sekta ya umma kwa asilimia 10 kwa mwaka huu vilevile kuuongeza umri wa kustaafu hadi miaka 63.

Wafanyakazi katika Wizara za serikali,mabaraza ya miji,hospitali,vyuo vikuu,mabenki na mahakama wote wanashiriki katika mgomo huo.Usafiri wa reli,ndege,barabarani na baharini umekwama.Waandishi wa habari nao pia wamegoma nchini humo. Illiad Stamels mwanachama wa chama cha wafanyakazi cha PAME.

anaeleza kuwa, ''Hali iliyoko sasa inawakilisha kunyanyaswa nchini mwetu.Vijana ndio watakaoathirika kwasababu ya mishahara kupunguzwa na kwa wakati huohuo mabenki yanalindwa ili yasilipe mabilioni ya kodi.Wanaojiweza hawatapata madhara ila wa tabaka la chini ndio watakaoumia.''alifafanua.

Hata hivyo baadhi ya waGiriki wenyewe wanaiunga mkono serikali kwa kuchukua hatua hizo.Asilimia 55 wako upande wa serikali ila asilimia 76 wengine wanaamini kuwa maandamano hayapaswi kufanyika mpaka pale nchi yao itakapoweza kujikwamua na matatizo hayo ya kiuchumi.Kulingana na wadadisi maandamano hayoleta tija kwa wawekezaji wa kimataifa ambao kwa sasa wameishusha thamani ya euro jambo ambalo limezifanya hisa za makampuni ya Ugiriki kupungua bei kwasababu ya hofu kwamba itashindwa kuyalipa madeni yake.

Screenshot faz.net Finanzkrise Griechenland Flash-Galerie

Maelezo ya hali halisi ya kiuchumi

Sarafu ya euro i hatarini

Wakati huohuo wataalam wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya,Benki ya jumuiya hiyo na Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF wote wamewasili mjini Athens ili kuzitathmini hatua zilizochukuliwa na serikali za kuipunguza nakisi ya bajeti yake.

Maafisa hao wa ngazi za juu wamekutana na kiongozi wa baraza la wataalam katika wizara ya fedha,George Zanias.Vikao vyengine vimepangwa kufanyika baadaye hii leo na kesho vitakavyowashirikisha maafisa wa wizara ya kazi na Benki ya Ugiriki.

Arbeitslose in Spanien Madrid

Wahispania wasiokuwa na kazi

Kwa upande mwengine mataifa mengine ya Ulaya nayo pia yanakumbwa na matatizo ya kiuchumi.Taarifa zinaeleza kuwa Italia ilichukua tahadhari zaidi kuyaficha maelezo ya hali yake ya kiuchumi ikilinganishwa na Ugiriki.Kulingana na Naibu Waziri Mkuu wa Italia Theodoros Pangalos,baadhi ya mataifa ya Ulaya yamelazimika kufanya hivyo ili kujinusuru.Maelfu ya raia wa Uhispania nao waliandamana ili kuipinga mipango ya serikali ya kuuongeza umri wa kustaafu.Hii ni mara ya kwanza vyama vya wafanyakazi vimeandaa mgomo wa kuipinga serikali.Serikali ya Uhispania inakabiliwa na tatizo kubwa kwasababu ya bajeti kubwa ya malipo ya uzeeni.

Matatizo ya fedha ya Ugiriki yameitumbukiza sarafu ya euro katika hali ngumu zaidi tangu ilipoundwa miaka 11 iliyopita.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-RTRE/DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 25.02.2010
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M9mE
 • Tarehe 25.02.2010
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/M9mE
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com