Maandamano Msumbiji. | Masuala ya Jamii | DW | 06.09.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Maandamano Msumbiji.

Watu 150 wamekamatwa na polisi kwa kuhusika katika vurugu.

default

Matairi ya magari yakiteketezwa mjini Maputo, Msumbiji.

Huduma za kutuma ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi nchini Msumbiji zimesitishwa hii leo, baada ya hapo awali kutumiwa kusambaza ujumbe wa kufanya maandamano kupinga kupandishwa bei za vyakula,maji,na huduma za umeme katika nchi hiyo iliyo maskini.

Maandamano hayo yaliofanyika katika mji mkuu wa Maputo wiki iliyopita, yaligeuka kuwa  vurugu zilizobabisha vifo vya watu wapatao10, waliopigwa risasi wakati wa mapambano na polisi

Redio ya taifa nchini humo hii leo imeripoti kukamatwa kwa watu takriban 150 kufuatia vurugu hizo.

Kituo hicho kimemnukuu msemaji wa polisi Joaquim Selemane, aliyesema kuwa polisi wanajaribu kuwatambua wahusika wakuu wa maandamano hayo yalioandaliwa kupitia ujumbe mfupi wa simu za mkononi,yaliosababisha kujeruhiwa kwa mamia ya watu.

Msemaji huyo alielezea redio hiyo kuwa, watu 142 walikamatwa kwa makosa ya kuchoma matairi ya magari na kusababaisha uharibifu wa mali, huku wengine sita wakishtumiwa kwa makosa ya kutuma ujumbe huo mfupi uliochochea vurugu hizo.

Kupandishwa kwa asilimia 30 kwa mkate kumesababisha hasira katika nchi hiyo ilio maskini,lakini serikali imekiri kuwa haina namna kutokana na kupanda kwa bei za ngano duniani.

Vyama vya upinzani na mashirika ya kutetea haki za binaadamu vimeishutumu serikali hiyo,vikieleza kuwa imeshindwa kutathmini hisia hizo za hasira kufuatia kupanda kwa bei za bidhaa hizo.

Ukame na moto uliowaka Urusi ambayo ni nchi ya tatu duniani inayoongoza kwa upanzi wa nafaka hiyo, na uamuzi wa serikali yake kuendeleza marufuku ya uuzaji wa bidhaa hiyo hadi mwaka ujao 2011, umechangia kuinuka maradufu kwa bei za ngano nchini Marekani kwa zaidi ya asilimia 25 mwaka huu.

Wachambuzi wanaeleza kuwa kupanda kwa bei za vyakula kutasababisha kupanda kwa gharama za maisha, lakini hatahivyo wanategema uekezaji wa rasilimali za nchi kutopungua.

Ijapokuwa Msumbiji ni nchi inayoinuka kwa haraka kiuchumi Barani Afrika, bado haijafufuka vilivyo kutokana na vita vilivyomalizika mwaka 1992.

Mwaka 2008 palishuhudiwa malalamiko na vurugu sehemu nyingi duniani,wakati bei za ngano na bidhaa nyingine za kilimo zilipopanda maradufu.

Mwandishi Maryam Abdalla/RTRE/APE

Mhariri.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com