1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liverpool wapeta, Man United na City hoi

7 Oktoba 2019

Liverpool wamejikuta katika nafasi nzuri sana ya kuwa na matumaini ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo ingawa msimu bado ni mchanga.

https://p.dw.com/p/3QqJh
UEFA Super Cup - Liverpool vs Chelsea
Picha: Reuters/J. Sibley

The reds walipata ushindi mgumu wa mabao mawili kwa moja walipochuana na Leicester Jumamosi uwanjani Anfield baada James Milner kufunga mkwaju wa penalti uliokuwa na utata katika dakika ya mwisho ya mechi baada ya Sadio Mane kuangushwa katika eneo la hatari.

Hapo Jumapili mabingwa Manchester City walilazwa magolimawili kwa bila walipokuwa wakikwaana na Wolves uwanjani Etihad nao mahasimu wa jadi wa Liverpool, Manchester United wakaaibishwa na Newcastle United moja bila.

Sasa Liverpool ambao hawajafungwa wala kutoka sare msimu huu wamefungua mwanya wa pointi nane wakiwa na pointi ishirini na nne huku Manchester City walio katika nafasi ya pili wakiwa na pointi kumi na sita.

Manchester United wao wako katika nafasi ya kumi na mbili pointi zao zikiwa tisa na wako pointi mbili tu kutoka eneo la kushushwa daraja na kocha wao Ole Gunnar Solksjaer anakiri wana kibarua kigumu.

"Tumejipa kibarua kigumu sana cha kuingia katika nafasi nne bora hata usizungumzie nafasi sita za kwanza na tunastahili kupata matokeo moja kwa moja. Tunastahili kushinda, klabu hii inastahili kushinda kila mechi lakini kwa sasa hatuezi hasa tunapocheza ugenini lakini tuna nafasi nzuri kabisa ya kuinua kiwango chetu cha mchezo na motisha wa mashabiki kwasababu mechi ijayo tunacheza na Liverpool," alisema Solksjaer.