″Linalompata Mubarak ni fundisho″ | Magazetini | DW | 14.04.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Linalompata Mubarak ni fundisho"

Magazeti ya leo yanazungumzia hatima ya sekta ya viwanda vya Japan, baada ya sehemu kubwa kuharibiwa na maafa yaliyoikumba nchi hiyo mwezi uliopita, majaaliwa ya Hosni Mubarak wa Misri, na sera ya uhamiaji ya Ujerumani.

Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak

Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anasema kuwa, janga la tetemeko la ardhi, tsunami na baadaye kuvuja kwa mionzi ya yuraniamu kutoka vinu vya nyuklia vya Fukushima, linaufanya ulimwengu uangaliane wenyewe kwa wenyewe.

Balaa hili, ambalo limegharimu takribani maisha ya watu 30,000, linahatarisha umadhubuti wa sekta ya viwanda nchini Japan, kwa sababu mbili: moja, miundombinu yake mingi na ya gharama kubwa imeharibiwa vibaya na, mbili, yanairudisha nchi hiyo nyuma katika vita vyake kwenye soko la bidhaa. Kwa mfano, viwanda vyake vya magari.

Kwa hali hii, mhariri anasema kuwa, ni jambo linalowezekana sasa, kwa kampuni ya magari ya Toyota ya Japan kujikuta ikipitwa haraka zaidi na kampuni ya Volkswagen ya hapa Ujerumani, maana sasa Volkswagen ina wasaa wa kujijenga kwenye soko, wakati Toyota ikijenga upya miundombinu yake.

Mhariri wa gazeti la Rheinische Post anazungumzia majaaliwa ya aliyekuwa rais wa Misri, Hosni Mubarak, ambaye hivi sasa, yeye na wanawe wawili wa kiume, wako chini ya kizuizi wakichunguzwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi.

Mhariri anasema kuwa mwisho wa maji ni tope. Kinachompata sasa Mubarak kinapaswa kuwa fundisho kwa watawala wote wa aina yake, kwamba hatimaye umma unaweza kuja kuinuka dhidi yao na kufikishwa mahala pabaya sana.

Uchunguzi wa sasa dhidi ya familia ya Mubarak ni ushindi kwa wapiganiaji demokrasia nchini Misri, ingawa si mwisho wa mapambano yao.

Hata hivyo, ifahamike kuwa wanachokitaka Wamisri hivi sasa ni haki ya kweli kutendeka na kuonekana kuwa inatendeka na si kiini-macho.

Mhariri anamalizia kwa kusema kuwakuta akina Milosevic, akina Mubarak, na pengine akina Gaddafi mbele ya mahakama ya sheria wakiwajibika kwa matendo yao, hapana shaka, ni habari njema.

Naye mhariri wa gazeti la Neue Westfälische anazungumzia sera na siasa ya uhamiaji wa Ujerumani, katika wakati ambao maelfu ya wakimbizi kutoka Afrika ya Kaskazini, wanaingia barani Ulaya kupitia kisiwa kinachomilikiwa na Italia cha Lampedusa.

Wimbi la wahamiaji wa Afrika ya Kaskazini kuingia Ulaya limewafanya wanasiasa wapate mada kufanyia siasa. Serikali ya Ujerumani inaiambia Italia: "Suala la wakimbizi hao ni lako mwenyewe, shughulika nalo kwa njia zako", na inaitisha wataalamu wafanye utafiti wa namna bora ya kulielekeza suala hili kwenye njia muwafaka.

Hili halina tafauti sana na ule msamiati wa serikali ya mseto ya weusi na manjano, usemao "wageni wazuri, wageni maudhi."

Msemaji wa siasa za ndani wa mseto huo, Hans-Peter Uhl, ameshasema kuwa "hatuwezi kugawana kiwango chetu cha maisha na wengine". Sababu ni kuwa hapa Ujerumani watu hudhani kuwa kila anayekimbilia hapa amekuja kutafuta kiwango kizuri cha maisha tu.

Hata hivyo, kuna ukweli mwengine hausemwi, kuwa Wajerumani wenye asili ya Kituruki waliosoma vizuri, huwa wanakimbilia Istanbul kufanya kazi na sio Ujerumani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/ZPR
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman