Leverkusen yalenga kucheza Champions League | Michezo | DW | 14.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Leverkusen yalenga kucheza Champions League

Bayer Leverkusen wamejirejesha tena katika nafasi ya kucheza kabumbu la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wao wa magoli mawili kwa moja nyumbani dhidi ya Hertha Berlin katika mechi ya Bundesliga

Huo ulikuwa mchuano wao wa kwanza katika Bundesliga tangu walipomtimua kocha Sami Hyyppia wiki iliyopita na kumtwika mzigo aliyekuwa msaidizi wake Sascha Lewandowski.

Akisheherekea ushindi wake wa kwanza, kocha Lewandowski alisema ipo kazi ya kufanywa kikosini kabla ya msimu kukamilika. "Bila shaka huwezi kutarajia kwamba sasa mambo yatakuwa mazuri sana kwa haraka. Lakini leo tumejituma. Nadhani nia na udhibiti wa mbinu zetu vilikuwepo. Pia unaona tunaelekea katika njia inayostahili, lakini pia unaona wazi kwamba tuna kazi nyingi ya kufanya ili kujiimarisha zaidi, hatua kwa hatua na kujipa nafasi nzuri ya kupata mafanikio katika mechi za mwisho."

Bayern walionekana kupunguza kasi tangu walipotawazwa washindi wa Bundesliga

Bayern walionekana kupunguza kasi tangu walipotawazwa washindi wa Bundesliga

Leverkusen ilifunga goli la kasi zaidi msimu huu katika Bundesliga, katika sekunde ya 40 wakati mshambuliaji Stefan Kiessling alipofungwa kwa kichwa, naye Julian Brandt akafanya mambo kuwa mawili katika dakika ya 24. Sandro Wagner aliifungia Berlin goli la kufutia machozi.

Ushindi huo umewaweka Leverkusen katika nafasi ya nne mbele ya Wolfsburg ambao waliwashinda Nuremberg magoli manne kwa moja. Nayo matumaini ya Augsburg kupata tikiti ya kucheza katika Europa League yalipata pigo wakati walipozabwa magoli mawili kwa sifuri na Hoffenheim.

Mabingwa Bayern nao walipata kipigo kingine cha pili mfululizo walipobamizwa magoli matatu kwa bila nyumbani na Borussia Dortmund uwanjani Allianz Arena. Henrikh Mkhitaryan, Marco Reus na Jonas Hofmann waliwazika Bayern ikiwa ni kichapo cha mara ya kwanza mjini Munich tangu 2012 na kikubwa zaidi tangu Septemba 2008.

Mabingwa hao wa Ulaya hawajashinda mechi yoyote kati ya tatu walizocheza kwenye ligi baada ya kutwaa taji la Bundesliga mwezi uliopita na ni mara ya kwanza tangu Novemba 2011 ambapo wameshindwa mara mbili mfululizo.

TSG 1899 Hoffenheim waliwabwaga FC Augsburg wanaotafuta nafasi katika Eruopa League

TSG 1899 Hoffenheim waliwabwaga FC Augsburg wanaotafuta nafasi katika Eruopa League

Manuel Neuer ni mlinda lango wa Bayern "Lilipozuka pambano dhidi ya Dortmund katika mkondo wa kwanza, kwa vile haikujulikana ni nani angekuwa mshindi wa ligi, tuliwashinda mabao mattau kwa bila. Na sasa hatujiumizi vichwa. Kwetu hili siyo tatizo sasa. Ni wazi tungetaka kuonyesha kitu kingine, hilo ni kweli, lakini hiyo haikuwa fainali kwetu".

Ushindi huo una maana nambari mbili Dortmund wamesonga pointi tatu mbele ya mahasimu wao Schalke 04, ambao wako katika nafasi ya tatu, na una maana kuwa wamejihakikishia kabisa nafasi ya kucheza katika Champions League msimu ujao. Jonas Hofmann ni mmoja wa wafungaji wa magoli ya BVB "Nadhani wengi hawakutarajia kwamba leo tungefanya mashambulizi makali hapa. Lakini ulikuwa mchezo mzuri sana. Siri ni kuwa tulikuwa na ulinzi mzuri na pia mchezo wetu ulikuwa mzuri, kutoka mbele hadi nyuma ya uwanja".

Borussia Moenchengladbach walianguka katika nafasi ya sita baada ya kutoka sare ya goli moja kwa moja nyumbani dhidi ya VfB Stuttgart wanaokabiliwa na kitisho cha kushushwa ngazi. Stuttgart sasa wako point moja mbele Ya nambari tatu kutoka nyuma Hamburg, ambao walifungwa magoli mawili kwa moja na Hanover 96. Katika mchuano mwingine wa timu mbili zinazong'ang'ana kutoiaga Bundesliga, Freiburg waliwazaba washika mkia Eintracht Braunswchweig magoli mawili kwa sifuri, wakati Mainz 05 wakiwasambaratisha Werder Bremen tatu bila.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdulrahman