1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Laporta: Nina imani Messi atasalia Barcelona

28 Mei 2021

Rais wa klabu ya Barcelona Joan Laporta ana matumaini kuwa staa wa klabu hiyo Lionel Messi atabaki klabuni humo licha ya kusalia na mwezi mmoja kwenye kandarasi yake.

https://p.dw.com/p/3u7de
Bildergalerie | Fussballer vor dem Wechsel 2021
Picha: Bagu Blanco/Shutterstock/imago images

Rais wa klabu ya Barcelona Joan Laporta ana matumaini kuwa staa wa klabu hiyo Lionel Messi atabaki klabuni humo licha ya kusalia na mwezi mmoja kwenye kandarasi yake.

"Messi atapewa mkataba mpya, lakini hilo bado halijafanyika,” Laporta ameuambia mkutano na waandishi wa habari leo Ijumaa, ukiwa ni mkutano wake wa kwanza tangu achukue mikoba ya Urais wa klabu hiyo kwa mara ya pili sasa.

Msimu uliopita, Messi alitaka kuondoka Barcelona baada ya klabu hiyo kutoshinda kombe lolote. Hata hivyo, mnamo Disemba mwaka jana alisema ataahirisha uamuzi juu ya klabu atakayoichezea baada ya msimu huu kukamilika.

Mkataba wa Messi unakamilika Juni 30.

Laporte amesema ana "matumaini ya kadri” kuwa yeye na Messi wanaweza kuafikiana juu ya mkataba mpya ambao utakubalika baina ya mchezaji mwenyewe na klabu.

Hata hivyo, Rais huyo wa Barcelona hakuweka wazi kiasi cha mshahara ambao Barcelona iko tayari kumlipa Messi, akisisitiza kuwa klabu hiyo bado inafanya tathmini ya ndani ya fedha zake kufuatia athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la Covid-19.

Msimu huu Barcelona ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya Uhispania La Liga, japo ilishinda kombe la Copa del Rey.

Akiwa Barcelona, Messi mwenye umri wa miaka 33 ameshinda mataji 10 ya ligi kuu ya Uhispania La Liga na mataji manne ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.