1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya miaka miwili tangu kifo cha Nkurunziza

8 Juni 2022

Burundi imeadhimishwa leo tarehe 08 Juni kumbukumbu ya mwaka wa pili tangu kufariki rais wa zamani wa Pierre Nkurunziza, Siku iliyotangazwa kuwa Siku ya Uzalendo.

https://p.dw.com/p/4CQd0
Burundi Wahlkampf Präsident Pierre Nkurunziza
Picha: AFP

Rais Evariste Ndayishimiye amesema mafunzo ya uzalendo yaliyoasisiwa na Pierre Nkurunziza yameanza kuzaa matunda ambapo baadhi ya watu wameanza kubadilika na kuipenda nchi yao, jina la ukimbizi likifutika kwa warundi na kuitwa warundi wanaoishi nje ya nchi. Hata hivyo amekosowa viongozi ambao bado wanajihusisha na ubadhirifu wa mali ya umma. 

Maadhimisho hayo ya mwaka wa pili tangu kufariki hayati Pierre Nkurunziza yamefanyika Gitega kwenye makao makuu ya kisiasa. Rais Evariste Ndayishimiye, akifuatiwa na mjane wa rais Nkurunziza, maafisa wa taasisi kuu za kitaifa na mabalozi wa nchi za kigeni hapa nchini wameweka mashada ya mauwa kwenye kaburi la hayati Pierre Nkurunziza.

Katika hotuba ya madhumuni rais Evariste Ndayishimiye amesema mafunzo ya uzalendo yaliyoasisiwa na hayati Nkurunziza yameanza kuzaa matunda. Rais amesema zipo dalili zinzazoonesha kuwepo na mabadiliko ikiwa ni pamoja na baadhi ya raia wakionekana  sasa kujirekebisha kwa kuachana na sera ya mtengano na ubaguzi, na wengine kusikitishwa na hali ngumu Burundi iliyopitia.

Burundi Vereidigung Präsident Evariste Ndayishimiye
Rais Evariste Ndayishimiye amesema mafunzo ya uzalendo yaliyoasisiwa na Pierre Nkurunziza yameanza kuzaa matunda Picha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Warundi waonekana kuwa sasa na moyo wa uzalendo, Kwanza wanaoichafua nchi yao si wengi kama ilivyo kuwa awali, pili raia sasa wanawapenda viongozi wao, hayo tunayashuhudia tunapoitembelea mikoa mbali mbali, na tunapozitembelea nchi za kigeni. Sera ya ubaguzi imekuwa ikitoweka.  Na isitoshi kumekuwa na raia wengi ambao wamekuwa wakitowa bila malipo fikra na maoni yanayochangia katika kuendeleza nchi#.

Rais Ndayishimiye amesema pia kuwa katika miaka hii raia waishio ugenini wamekuwa wakijenga majumba ya kifahari nchini, hali inayopelekea wawekezaji wa kigeni kuvutiwa na kuja kuwekeza Burundi.

Pia amesema jina la wakimbizi limeanza kutoweka na hivyo warundi kuitwa raia waishio ugenini.

Licha ya hatua hiyo ya kupendeza katika kuimarika  uzalendo,  rais Ndayishimiye amesema bado kunashuhudiwa raia na hususan viongozi wasiowajibika katika majukumu yao. Baadhi hujihusisha hata na ubadhirifu wa mali ya umma.

Rais Ndayishimiye ametumia fursa hii kuwataka wale ambao bado wamesalia nyuma kuiga mfano wa mababu.

Pierre Nkurunziza aliyeiongoza Burundi kwa kipindi cha miaka 15, na alifariki Juni 08 mwaka 2020, anakumbukwa zaidi kwa kuazimia wanawake waja wazito kujifungua pasina malipo, watoto wenye hadi umri wa miaka 5 kupewa matibabu bure na wanafunzi wa shule za msingi kusoma bila malipo hatua ambazo zinaendelea kuzingatiwa.

Amida ISSA, DW BUJUMBURA