Kongamano la UKIMWI laanza Amsterdam | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.07.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kongamano la UKIMWI laanza Amsterdam

Kongamano la kimataifa la UKIMWI linaanza leo Jumatatu mjini Amsterdam likiwa na matumaini ya kuendeleza harakati za mwanamuziki wa kimataifa Elton John na Prince Harry dhidi ya maradhi hayo.

UNAIDS Generalsekretär Peter Piot AIDS-Report

Maelfu ya wajumbe wakiwemo watafiti, wanaharakati pamoja na watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanatarajia kushiriki kongamano hilo la 22 la kimataifa.

Katika siku za hivi karibuni wataalamu wametahadharisha kuwa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi yameongezeka kwa kasi katika baadhi ya maeneo  duniani kutokana na hatua za kupambana na maradhi hayo  kupungua pamoja na kushuka kwa ufadhili.

Aidha wataalamu wamelalamika juu ya kupungua kwa mkazo katika juhudi za kuzuia kuenea maradhi ya ukimwi ikiwa ni pamoja na kugawa mipira ya kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi wakati wa tendo la kujamiiana hali inayochangia kusambaa kirahisi virusi vya ukimwi.

Peter Piot, mtafiti wa virusi vinavyosababisha maradhi ya ukimwi na muasisi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika kupambana  kuenea kwa   maradhi ya UKIMWI -UNAIDS alisema wiki iliyopita   hatua iliyoonekana katika kipindi cha muongo mmoja uliopita ikionesha kupungua  maambukizi mapya  imewafanya baadhi kuamini  dunia iko katika hatua ya kudhibiti maradhi ya ukimwi. 

Hata hivyo amesisitiza na kuonya kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha matumaini hayo.

Ripoti ya UNAIDS imeonya juu ya safari ndefu na ngumu  iliyopo ya kudhibiti kuenea  maradhi hayo ingawa shirika hilo limeripoti kupungua  maambukizi mapya  na vifo vitokanavyo na maradhi ya ukimwi ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.

 

UN yasema mafanikio hayaendelezwi

Flash-Galerie AIDS Projekte

Mmoja wa wanaharakati akionesha bango wakati akishiriki semina kuhusu virusi vya UKIMWI.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema  mafanikio yaliyofikiwa katika kupunguza maambukizi dhidi ya watoto hayaendelezwi. 

Aidha wakati wakiwa katika matayarisho ya mwisho kwa ajili ya kongamano hilo la ukimwi la siku tano  litakalojumuisha watu 15,000 wakiwemo watu mashuhuri, wataalamu wameonya kuwa mafanikio haya yaliyopatikana kwa tabu yanaweza kuwa kinyume chake iwapo hali haitabadilika katika juhudi za kudhibiti maradhi hayo.

Mark Dybul mtafiti mwandamizi wa virusi vya  ukimwi nchini Marekani ameonya  kuongezeka kwa kasi ya maambukizi mapya  miongoni mwa kundi la vijana  katika nchi zilizoatahiriwa zaidi  kunatishia kuongezeka kwa watu walio na virusi vya ukimwi.

 Akizungumza katika mkutano kabla ya kuanza kwa kongamano hilo Dybul  ameonaya kuwa  hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo hakutakuwa na fedha na kuwa ulimwengu uko katika hatari ya kushindwa kudhibiti kuongezeka maradhi ya ukimwi.

Mark Dybul amesema misaada ya wafadhili na ufadhili wa ndani nao pia umepungua  na unaweza kuendelea kupungua  kutoka kiasi cha dola bilioni 24.1 mwaka jana  huku kiasi kikubwa cha fedha hizo zikifadhiliwa kwa bajeti ya ndani ya mataifa yaliyoathiriwa zaidi na maradhi ya ukimwi.  Kwa mujibu wa UNAIDS kuna upungufu wa dola bilioni 7 kwa mwaka.

Hayo yanajiri mnamo wakati chini ya utawala wa sasa rais  Donald Trump wa Marekani ukipendekeza kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya kupambana dhidi ya virusi vya UKIMWI ingawa hoja hiyo imeshindwa kupita katika bunge la Congress.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Josephat Charo