1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Kongamano la kuichangia fedha Sudan lafanyika Ufaransa

Amina Mjahid
15 Aprili 2024

Wanadiplomasia wakuu kutoka Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Ulaya, wanatarajiwa kuchangisha fedha zaidi kwa ajili ya Sudan.

https://p.dw.com/p/4em06
Mkutano kuhusu Sudan unaofanyika Ufaransa
Mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya Sudan unaofanyika mjini Paris, Ufaransa. Picha: Christophe Ena/dpa/AP/picture alliance

Juhudi hizo ni kupitia kongamano la wafadhili linalofanyika leo mjini Paris Ufaransa, ambapo ni mwaka mmoja tangu mzozo wa Sudan kuzuka Aprili 15, baada ya mvutano wa muda mrefu kuzuka na kusababisha mapigano makali kati ya jeshi na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF)

Shirika la habari la Reuters limesema Marekani inapanga kutangaza fedha zaidi ya dola milioni 100 za msaada katika kongamano hilo linalotarajiwa kuhudhuriwa na Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné, mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell na Kamishna wa Umoja huo wa shughuli za usimamizi wa migogoro Janez Lenarcic.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimeharibu vibaya miundombinu, kuiweka nchi hiyo katika hatari ya kukabiliwa na baa la njaa na kusababisha raia wengi kupoteza makaazi yao.