1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha wa Dortmund Marco Rose apigwa kalamu

20 Mei 2022

Klabu ya Borussia Dortmund imemfuta kazi kocha Marco Rose baada ya klabu hiyo kushindwa kushinda kombe lolote msimu huu. Akiwa Dortmund, amesimamia mechi 46 huku akishinda mechi 27, kutoka sare 4 na kufungwa mechi 15.

https://p.dw.com/p/4BdPN
Marco Rose Trainer Borussia Dortmund
Picha: Stefan Matzke/sampics/picture alliance

Dortmund imesema uamuzi wa kumfuta kazi Rose ulifuatia mkutano wa kutathmini mafanikio ya msimu uliomuhusisha Marco Rose na viongozi wakuu wa klabu akiwemo afisa mkuu mtendaji Hans-Joachim Watzke mnamo Alhamisi.

Rose mwenye umri wa miaka 45, alichukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya Signal Iduna Park mwaka 2021, na kabla ya hapo aliwahi kuzifunza Red Bull Salzburg na Borussia Monchengladbach.

Taarifa kutoka Dortmund imesema: "BvB na Marco Rose wameamua kumaliza uhusiano wao. Kufuatia tathmini ya kina ya msimu huu, klabu imeamua kusonga mbele na inamtakia Marco Rose kila la kheri."

Borussia Dortmund inanuia kuiwekea shinikizo Bayern Munich msimu ujao katika mbio za ubingwa na tayari imesajili wachezaji watatu akiwemo mshambuliaji Karim Adeyemi, na mabeki Nico Schlotterbeck na Niklas Süle.

Hata hivyo, mshambuliaji wa kutegemewa Erling Haaland amejiunga na Manchester City huku kiungo Axel Witsel akiondoka.