Kocha Bayern asema Real Madrid wanapigika | Michezo | DW | 26.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kocha Bayern asema Real Madrid wanapigika

Bayern Munich ilipoteza nafasi kadhaa katika kipigo chao cha magoli 2-1 nyumbani dhidi ya Real Madrid katika duru ya kwanza ya nusu fainali ya Champions League, lakini Kocha Jupp Heynckes amesema bado wana matumaini.

Bayern walipaswa kuongoza kwa magoli kadhaa katika kipindi cha kwanza kutokana na fursa walizokuwa nazo Thomas Mueller, Robert Lewandowski, Mats Himmel na Franl Ribery.

Lakini Wajerumani hao waliangushwa na umalizaji mbaya isivyo kawaida, uliowaruhusu mabingwa watetezi Real Madrid kuchomoka na ushindi na kuwaacha Bayern katika hatari ya kuondolewa mashindanoni na klabu ya Uhispania kwa msimu wa tano mfululizo.

"Hatukati tamaa," alisema Heynckes, aliyeiongoza Bayern katika ushindi wa mataji matatu mwaka 2013. " Unapotengezena nafasi nyingi dhidi ya timu kama Real basi hii ni ishara pia kwamba hasimu wako anapigika."

"Hatuna cha kupoteza na tutacheza kwa uhuru. Pengine zaidi ya tulivyocheza katika duru ya kwanza kwa sababu mchezo wetu haukuwa imara kama ambavyo tungependa."

UEFA Champions League Halbfinale | FC Bayern München - Real Madrid | TOR Madrid (Reuters/M. Rehle)

Real Madrid wakifunga goli lao la kwanza kupitia kwa Marcelo, katika uwanja wa Alllianz Arena mjini Munich, Aprili 25,2018.

Majeraha ya mapema yawaponza

Bayern ilipata matatizo ya mapema kutokana na majeraha kwa Arjen Robben na Jerome Boateng lakini waliendelea kupenya ngome ya Real kwa urahisi katika dakika 45 za kwanza, huku walinzi wa klabu hiyo ya Uhispania wakipambana na kasi ya Ribery na Lewandowski.

Lakini badala ya kuongezea kwenye goli la ufunguzi la Joshua Kimmich alilolipachika wavuni katika dakika ya 28, walikubali goli la kusawazisha dakika ya 44 kupitia mkwaju uliopigwa kwa ustadi na Marcelo, baada ya Dani Carvajal kuupiga mpira kwa kichwa na kuangukia karibu na eneo alilokuwa Marcelo.

Baadaye kosa la kiulinzi lililofanywa na Rafinha liliwaruhusu real kufunga bao la ushindi na kuiacha Bayern ikihitaji ushindi mjini Madrid wiki ijayo ili kusonga mbele katika hatua ya fainali.

"Simlaumu yeyote lakini operesheni zetu za ulinzi katika magoli yote zilikuwa mbaya," alisema Heynckes. Umalizaji wetu pia haukuwa mzuri. Hatukuwa na umakini kama kawaida yetu."

Bado kukata tamaa

Bayern ilikuwa haijafanya makosa mengi katika msimu huu wa 2018, ikiwa imefunga magoli 69 katika mechi zao 20 katika mashindano yote hadi Jumatano.

Champions League - FC Bayern München v Real Madrid (picture-alliance/GES/M. Gilliar)

Bayern wakiondoka uwanjani vichwa chini baada ya kipigo cha 2-1 kutoka kwa Real Madrid.

Heynckes alishinda mechi zake 12 mfululizo za ligi ya mabingwa barani Ulaya, Chamapions League, huku Bayern ikiwa imepoteza mara moja katika mechi ya nyumbani katika mechi zake 22 za mwisho za nyumbani kwenye mashindano kuelekea mechi ya Jumatano. Kipigo hicho kimoja hata hivyo, kilikuwa dhidi ya Real Madrid katika robo fainali ya mwaka jana.

"Mwisho wa siku ni 2-1 kwa Real na hatukujifanyia vyema," alisema nahodha wa Bayern Thomas Mueller. "Namna walivyotimiza hilo (Real) ni suala lao lakini inaonyesha kwamba bado kuna nafasi kubwa katika duru ya duru ya pili."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.

Mhariri: Josephata Charo.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com