1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha Navalny kulishwa sumu chazidisha wasiwasi

Admin.WagnerD3 Septemba 2020

Shirika la kudhibiti matumizi ya Silaha za Sumu OPCW limeelezea wasiwasi mkubwa baada ya Ujerumani kusema kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny alipewa sumu aina ya Novichok, inayoua mishipa.

https://p.dw.com/p/3hxS2
Russland Moskau Nawalny
Picha: Reuters/T. Makeyeva

Mkuu wa OPCW, Fernando Arias amesema shirika hilo lenye makao yake mjini The Hague lilikuwa tayari kusaidia taifa lolote mwanachama atakayehitaji msaada wake.

Mapema, ikulu ya Kremlin kupitia msemaji wake Dmitry Peskov imeyakana madai hayo, huku miito ya kimataifa ikiongezeka ya kuchukuliwa hatua dhidi ya Urusi. Amesema, Berlin haijatoa uthibitisho na kuongeza kuwa hakuna sababu ya kulituhumu taifa hilo, lakini pia akikataa mazungumzo kuhusiana na vikwazo vya kiuchumi huku akiyataka mataifa ya magharibi kutokimbilia kuwahukumu.

Berlin ilisema Navalny alipewa sumu ya jamii ya Novichok, sawa na ile iliyotumika dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi na Uingereza, Sergei Skripal pamoja na binti yake katika mji wa Salisbury nchini Uingereza miaka miwili iliyopita, hatua iliyoibua miito ya kulaani na kushinikiza uchunguzi zaidi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameyarudia matamshi yake kwamba hatua yoyote itakayochukuliwa na Ujerumani ama Umoja wa Ulaya kuhusiana na ufichuzi huo, itategemeana na iwapo Urusi itasaidia kuondoa kiwingu kilichopo.

Deutschland Merkel PK Navalny
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/M. Schreiber

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri mkuu wa Sweden Stefan Loefven mjini Berlin, Merkel amesema hana la kuongeza baada ya taarifa aliyoitoa jana kuhusiana na jaribio hilo la kumuua Navalny.

"Merkel: Bila shaka ninafuatilia kinachoelezwa, lakini ninapenda kusema kwamba siku ya jana nilitoa msimamo mpana kuhusu kile tutakachokifanya sasa na siku zijazo. Na kwa hakika, inategemea sana namna serikali ya Urusi itakavyojibu. Lakini sina cha kuongeza kwenye maneno yangu ya jana."

Huku hayo yakiendelea, rais wa Belarus Alexander Lukashenko amedai kwamba vikosi vyake vya usalama vimeingilia mazungumzo ya simu ya Ujerumani na kuonyesha kwamba madai hayo yalikuwa ni ya uongo.

Lukashenko amemwambia waziri mkuu wa Urusi Mikhail Mishustin aliyeko ziarani mjini Minsk kwamba mawasiliano ya simu kati ya Berlin na Warsaw yalionyesha tukio hilo lilikuwa na kutunga. Aliwanuukuu wazungumzaji aliodai walisema "Wamefanikisha, ili kumvunja moyo rais Vladmir Putin wa Urusi ili asiendelee kujiingiza kwenye masuala ya Belarus. Hata hivyo hakufafanua zaidi.

Uingereza kupitia waziri wake wa mambo ya kigeni, Dominic Raab, imesema Urusi ina swali zito la kujibu kuhusiana na madai hayo na ameahidi kuisaidia Ujerumani na washirika wengine wa kimataifa kuhusiana na suala hilo.