1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChad

Kiongozi wa upinzani Chad auawa katika shambulizi la kijeshi

Grace Kabogo
29 Februari 2024

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Chad, Yaya Dillo ameuwawa katika makabiliano ya risasi na vikosi vya usalama karibu na makao makuu ya chama chake mjini N'Djamena, huku hali ya wasiwasi wa kisiasa ikitawala.

https://p.dw.com/p/4d2Hf
Kiongozi mkuu wa upinzani Chad, Yaya Dillo
Kiongozi mkuu wa upinzani Chad, Yaya DilloPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali Abderaman Koulamallah, amesema Alhamisi kuwa Dillo aliuawa Jumatano kwenye makao makuu ya chama cha Wasoshalisti Wasiojali Mipaka, PSF, baada ya kukimbilia huko na kujifungia.

Koulamallah ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano amesema Dillo alikataa kujisalimisha na aliwafyatulia risasi askari.

Mazingira ya kifo cha Dillo hayajaelezwa

Mapema Alhamisi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Chad, Oumar Mahamat Kedelaye aliwataja waliouawa katika shambulizi hilo akiwemo Dillo bila kutoa maelezo zaidi kuhusu mazingira ya vifo hivyo.

Dillo alishutumiwa na serikali kwa kuongoza shambulizi dhidi ya ofisi ya idara ya usalama wa ndani usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano.

Barabara kuelekea ofisi za PSF, N'Djamena ikiwa imezingirwa na jeshi
Barabara kuelekea ofisi za PSF, N'Djamena ikiwa imezingirwa na jeshiPicha: AFP/Getty Images

Hata hivyo, akizungumza Jumatano na shirika la habari la Ufaransa, AFP, Dillo alikanusha kuhusika na shambulizi hilo, akiziita shutuma hizo za "uwongo", na zilizochochewa kisiasa, akisema hakuwepo wakati mkasa huo ukitokea.

Jana milio ya risasi za kivita ilisikika karibu na makao makuu ya chama cha PSF, kwenye mji mkuu wa Chad, N'Djamena.

Utulivu warejea N'Djamena

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa hali ya utulivu imerejea Alhamisi asubuhi kwenye mji mkuu N'Djamena na wakaazi walianza kwenda kazini, huku kukiwa na idadi ndogo ya wanajeshi wanaoonekana mitaani, ingawa mtandao wa intaneti, ambao ulizuiwa siku moja kabla bado haujarudi.

Siku ya Jumanne, Chad ilitangaza kuwa uchaguzi wa uraisi utafanyika Mei 6, ambapo rais wa mpito Mahamat Idriss Deby Itno na Dillo ambao ni mabinamu, wote walikuwa wanapanga kugombea.

Rais wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno
Rais wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno Picha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Taarifa ya serikali ilisema kuwa idara ya usalama ilishambuliwa na wawaskilishi wa chama cha Dillo, na kusababisha vifo kadhaa.

Mwanachama wa PSF auawa

Katika tukio jingine, serikali imesema mwanachama mmoja wa chama cha PSF, Ahmed Torabi alifanya jaribio la mauaji dhidi ya Rais wa Mahakama ya Juu, Samir Adam Annour.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Torabi aliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Jumanne na mwili wake uliwekwa kwenye makao makuu ya idara hiyo.

Mwezi Desemba, Mahakama ya Juu ya Chad iliidhinisha kura kuhusu katiba mpya ambayo wakosoaji wanasema ingeweza kusaidia kuimarisha mamlaka ya kiongozi wa kijeshi, Mahamat Idriss Deby.

 

(AFP, Reuters)