1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChad

Chad yaendesha msako baada ya shambulizi la idara ya usalama

Grace Kabogo
29 Februari 2024

Vikosi vya usalama vya Chad vinaendelea na msako mkali kwenye mji mkuu N'Djamena baada ya milio ya risasi kusikika karibu na makao makuu ya chama kikuu cha upinzani.

https://p.dw.com/p/4d0uw
Askari polisi wa Chad
Askari polisi wa ChadPicha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Msako huo unafanyika siku moja baada ya serikali ya Chad kusema kuwa watu kadhaa wameuawa katika shambulizi dhidi ya ofisi ya idara ya usalama wa ndani na kuwatuhumu wale iliyowataja kuwa wanachama wa upinzani kuhusika. 

Milio ya risasi iliyosikika mapema Jumatano ilisababisha watu kuondoka kwenye eneo hilo lililoko katikati ya mji wa N'Djamena ambako jeshi lilikuwa limeyazingira makao makuu ya chama cha Wasoshalisti Wasiojali Mipaka, PSF. Magari yaliyokuwa na walinzi wa rais pia yalionekana kuelekea kwenye ofisi hizo.

Serikali inakishutumu chama cha PSF kwa kuhusika na shambulizi katika ofisi ya idara ya usalama wa ndani mapema wiki hii, ambalo lilisababisha mauaji ya watu kadhaa.

Kiongozi wa chama cha PSF, Yaya Dillo na mpinzani mkubwa wa Rais wa Mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno, amekanusha kuhusika katika shambulizi hilo la Jumanne usiku.

Kiongozi wa chama cha PSF, Yaya Dillo
Kiongozi wa chama cha PSF, Yaya Dillo Picha: privat

Akizungumza na shirika la habari la Ufaransa, AFP, Dillo ambaye pia ni binamu wa Deby, amezitaja shutuma hizo kama za "uwongo", akisema hakuwepo wakati mkasa huo ukitokea. Dillo amesema lengo la serikali ni kumzuia, na kumtisha ili asigombee uchaguzi.

Shambulizi hilo limefanyika siku moja baada ya kutangazwa kuwa uchaguzi wa Chad utafanyika Mei 6, uchaguzi ambao Deby na Dillo wote wanakusudia kugombea.

Serikali yatoa onyo

Taarifa ya serikali iliyotolewa na kusomwa Jumatano usiku kwenye televevisheni ya taifa imeeleza kuwa serikali inapenda kuujulisha umma kwamba shambulizi hilo limefanywa kwa makusudi na washirika wa PSF, wakiongozwa na kiongozi wa vuguvugu hilo, Yaya Dillo.

Taarifa hiyo ilisomwa na mtangazaji wa televisheni hiyo, Remadji Horion Odette. "Ni muhimu kusisitiza kwamba yeyote anayetaka kuvuruga mchakato wa kidemokrasia unaoendelea nchini, atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo," alifafanua Remadji katika taarifa hiyo ya serikali.

Mji mkuu wa Chad, N'Djamena
Mji mkuu wa Chad, N'DjamenaPicha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya serikali baada ya shambulizi la ofisi za idara ya usalama, mwanachama wa PSF alikamatwa na kutuhumiwa kwa jaribio la mauaji dhidi ya rais wa mahaka ya juu.

Umoja wa Mataifa unafuatilia hali inayoendelea

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika ya Kati, amesema katika taarifa yake kuwa anafuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea Chad na ametoa wito kwa wadau kuwa na ustahimilivu na kujizuia.

Waziri Mkuu wa Chad, Succes Masra amezungumzia hali mbaya inayoendelea. Masra kiongozi wa zamani wa upinzani, ambaye hivi karibuni ameteuliwa na rais wa mpito, ameandika katika mtandao wa X kuwa anaonyesha uungaji mkono wake kamili na usio na masharti kwa mkuu wa nchi na vikosi vya ulinzi.

Kulingana na waandishi habari wa AFP, tangu jana mchana, huduma za simu na mtandao wa intaneti zilitatizwa.

(AFP, Reuters)