1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kibaki amteua Kalonzo kuwa makamu wake.

8 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cmbd

Nairobi. Mwenyekiti wa umoja wa Afrika rais John Kufour wa Ghana anakwenda nchini Kenya leo kusaidia kuumaliza mzozo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 500. Lakini matumaini ya kufikiwa kwa suluhisho la haraka katika mzozo huo , yamepungua leo , wakati serikali na upinzani wakiwa bado wamegawika juu ya jinsi ya kuendesha majadiliano hayo.

Wakati pande hizo mbili zinaendelea na mvutano kwa mshangao mkubwa wa Wakenya wengi wa kawaida, waziri wa fedha Amos Kimunya amesema kuwa ghasia zinaweza kuigharimu nchi hiyo zaidi ya dola bilioni moja.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga na rais Mwai Kibaki wanakabiliwa na mbinyo mkali wa kimataifa ili kuweza kukutana ana kwa ana , lakini wanaonekana kuwa wanasigana juu ya vipi hali hiyo inawezekana kutokea.

Kibaki amesema yuko tayari kuunda serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi uliomuweka tena madarakani hapo Desemba 27, ambao umesababisha mvutano mkubwa. Kwa upande wake Odinga anadai kuwa Kibaki ameiba kura na anapaswa kujiuzulu kutoka madarakani, na kufanya mazungumzo kupitia mpatanishi wa kimataifa na kuingia katika utaratibu wa utawala wa mpito kabla ya kufanyika uchaguzi mpya. Lakini serikali ya Kenya ambayo imekuwa ikizuia upatanishi wa kimataifa , imesema kuwa Kufour ataondoka kesho Jumatano na imemualika Odinga kwa mazungumzo hapo siku ya Ijumaa.