Kenya yatangaza siku saba za maombolezo kufuatia kifo cha Magufuli | Matukio ya Afrika | DW | 18.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Kenya yatangaza siku saba za maombolezo kufuatia kifo cha Magufuli

Kenya imetangaza maombolezo ya siku 7 ya kitaifa kufuatia kifo cha rais wa nchi jirani ya Tanzania John Pombe Magufuli.

Rais Uhuru Kenyatta ameamuru bendera kupeperushwa nusu mlingoti kote nchini na kwenye balozi zake zote kuanzia leo hadi siku atakayozikwa marehemu Rais Magufuli.

Kwenye taarifa yake aliyoitoa akiwa Ikulu ya Nairobi Rais Uhuru Kenyatta ametangaza maombolezi ya kitaifa ya wiki nzima kwa wakenya wote. Kadhalika ameamuru bendera kupeperushwa nusu mlingoti ndani na nje ya mipaka ya nchi na kwenye balozi zote za Kenya.

Bendera zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia asubuhi hadi jua litakapotua kutokea leo hadi siku atakayozikwa marehemu Rais Magufuli. Rais Uhuru alisikitishwa na kifo hicho na kumtaja marehemu kama kiongozi shupavu aliyeiongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuweka mbele maslahi ya Watanzania.

"Nakumbuka haswa safari yake rasmi ya Kenya ambapo alitutembelea hapa Kenya na tukaifungua pamoja barabara ya Southern Bypass. Kwangu mimi binafsi alinipatia heshima kubwa sana kwa kusisitiza ya kwamba lazima amtembelee mamangu Mama Ngina Kenyatta. Na pia mimi alinialika nikapata nafasi ya kumtembelea mamake mzazi huko Chato.Tulilala kwake nyumbani. Nimempoteza kiongozi mwenzangu. Sisi na wananchi wa wakenya tunasimama na  wenzetu wa Tanzania katika kipindi hiki kigumu," amesema Rais.

Kabla ya kifo chake, marehemu rais Magufuli alikuwa anahudumu kwenye muhula wa pili wa kiongozi wa tano wa Tanzania.Itakumbukwa kuwa tarehe 10 mwezi wa Machi serikali ya Kenya ilikanusha tetesi kuwa marehemu rais Magufuli alikuwa anatibiwa nchini Kenya.

Viongozi wa kisiasa watuma risala za rambirambi

Wakati huo huo, kiongozi wa upinzani wa ODM Raila Odinga ametuma rambirambi kwa familia ya marehemu Rais Magufuli.

Raila Odinga na marehemu Rais Magufuli walikuwa wandani wa karibu na wamekuwa wakisimama pamoja kwenye shughuli za kifamilia na binafsi. Mjumbe huyo wa umoja wa afrika AU, anawatolea wito watanzania kudumisha amani hasa katika kipindi hiki cha kubadili madaraka.

Kwa upande mwengine Kiongozi wa chama cha upinzani cha Amani Musalia Mudavadi ametiwa huzuni na na kifo hicho na kuwatakia watanzania amani wanapomuenzi kiongozi wao aliyepambana na rushwa na kuufanyia kazi uchumi wa taifa hilo.

Makamu wa rais wa Kenya wa zamani na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alituma rambirambi zake na kuwaombea watanzania katuka kipindi hiki kigumu.

Magavana wa kaunti kadha wa kadha akiwemo mwenyekiti wa baraza lao aliye pia gavana wa Embu Martin Wambora amesema wanaungana na watanzania kumuomboleza kiongozi aliyemtaja kuwa wa kipekee.