1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL : Wakorea wawili waachiliwa huru

14 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZR

Wanawake wawili wa Korea Kusini waliotekwa nyara na kundi la Taliban wameachiliwa huru nchini Afghanistan baada ya kuwa kizuzini kwa zaidi ya wiki tatu.

Msemaji wa Taliban amesema wanawake hao wameachiliwa kama ishara ya nia njema.Hata hivyo wenzao 19 bado wanaendelea kushikiliwa mateka na Rais wa Korea Kusini amesema kwamba serikali yake itafanya kila jitihada kuhakikiswa kwamba Wakorea hao wanaachiliwa huru.

Huo ni ufumbuzi wa kwanza mkuu tokea kuanza kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Korea Kusini na wanamgambo hao wa itikadi kali.Taliban tayari imewauwa Wakorea wawili na imekuwa ikidai kuachiliwa kwa wafungwa wa Taliban ili kubadilishana na Wakorea 19 waliobakia.

Mjerumani mmoja pia anaendelea kushikiliwa mateka na kundi la Taliban.Thomas Ruttig mtaalamu kwa Afghanistan wa Wakfu wa Siasa na Sayansi wa Ujerumani akizungumzia suala la mateka huyo anasema:

(O-TON Ruttig)

Anasema anafikiri kunapaswa pia kuwepo shinikizo ili kwamba mazungumzo yaharakishwe kadri inavyowezekana na kumalizika kwa haraka na kwamba wanalazimika kukubali kuwa iwapo mtu anashindwa kuwafanya Taliban wazungumze kundi hilo litakuja kukosa subira juu ya sakata hilo na angelipenda suala hili limalizike.

Katika simu iliopigwa kwa shirika moja la habari mtu aliyejitambulisha kuwa mateka wa Kijerumani anayeshikiliwa nchini Afghanistan kwa zaidi ya wiki tatu amesema kwamba watekaji wake wa Taliban wanataka kumuuwa.

Mwanaume huyo amesema kwamba ni mgonjwa na ameisihi serikali ya Ujerumani imsaidie.