Juncker: Umoja wa Ulaya haupaswi kutishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Juncker: Umoja wa Ulaya haupaswi kutishwa

Jean-Claude Juncker amesema anajiamini kuwa atakuwa rais mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya licha ya onyo la Waziri Mkuu wa Uingereza kwamba jambo hilo litapelekea kujitowa kwa Uingereza kwenye umoja huo.

Jean-Claude Juncker mgombea urais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.

Jean-Claude Juncker mgombea urais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu huyo wa zamani muhafidhina wa Luxembourg amesema katika mahojiano yaliyochapishwa Jumapili (01.06.2014) na gazeti la Bild am Sonntag kwamba "Ulaya haipaswi kutishwa".

Juncker ameongeza kusema kwamba amepata uungaji mkono mkono mkubwa kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya kutoka pande zote mbili za wahafidhina na wasoshalisti kushika wadhifa wa kuuongoza Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 28 na kwamba anaweza kuanza kushika wadhifa huo katikati ya mwezi wa Julai.

Gazeti la Ujerumani la Der Spiegel liliripoti hapo awali kwamba Cameron aliwaambia wanasiasa kadhaa akiwemo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwamba uteuzi wa Juncker kwa wadhifa huo utaiyumbisha serikali ya Uingereza kiasi cha kufanya kura ya maoni iliopangwa kuhusu uwanachama wake kwa Umoja wa Ulaya iitishwe kwa haraka zaidi na kwamba uwezekano wa kura ya hapana utazaidi kupata mshiko.

Vyama vyote viwili vya Merkel na Juncker ni wanachama wa chama cha mrengo wa kati kulia cha Wananchi barani Ulaya (EPP) ambalo ni kundi la kisiasa lililojizolea wingi wa viti katika uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya wiki iliopita.

Cameron anampinga Juncker

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Gazeti la Spiegel limesema kwamba Cameron alielezea pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Jumanne iliopita kwamba iwapo Juncker atakuwa rais wa halmashauri hiyo hatoweza tena kuhakikisha kuendelea kwa uwanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Matamshi yake yamechukuliwa kumaanisha kwamba kura ya maoni juu ya Uingereza kubakia katika Umoja wa Ulaya au kujitowa itabidi iitishwe na mapema ambapo yumkini ikapalekea wananchi wa Uingereza kujitowa katika umoja huo.Msemaji katika ofisi ya waziri mkuu huyo amekataa kuzungumzia juu ya makala ya gazeti hilo.

Gazeti hilo limesema Cameron ambaye anamuona Juncker kuwa ni mtu mwenye msimamo mkali wa kupendelea muungano wa Umoja wa Ulaya na yumkini akavuruga matarajio yake ya kurekebisha uhusiano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya, amepuuza ugombea wa Juncker wa wadhifa huo kwa kutumia maneno "Sura ya miaka ya thamanini haiwezi kutatuwa matatizo ya miaka mitano ijayo."

Kura ya maoni Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Cameron ameahidi kujadili upya masharti ya Uingereza kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya na iwapo chama chake cha Kihafidhina kitashinda katika uchaguzi mkuu wa taifa mwaka 2015 ataitisha kura ya maoni kuhusu iwapo nchi hiyo iendelee kubakia Umoja wa Ulaya ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017.

Jumatatu iliopita alikataa wito wa kuitisha kura hiyo ya maoni na mapema baada ya chama chake kushindwa na kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya ambapo chama kinachopinga Umoja wa Ulaya cha UK Independence (UKIP) kilishika nafasi ya kwanza.

Gazeti la Bild am Sonntag ambalo halikutaja duru zake limesema kwamba Rais Francois Hollande wa Ufaransa pia alikuwa amejaribu kuzuwiya Juncker kupata wadhifa huo wa rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na badala yake alipendekeza waziri wake wa zamani wa fedha Pierre Moscovici ashike wadhifa huo.

Juncker sio mgombea pekee

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi.

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi.

Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi amesema kunahitajika majadiliano ya kisiasa kuamuwa nani atakuwa rais mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na kwamba Juncker sio mgombea pekee.

Akizungumza katika mkutano wa kiuchumi katika mji wa kaskazini wa Italia wa Trento Jumapili kiongozi huyo wa sera za mrengo wa kati kushoto amesema kwamba kwa vyovyote vile Juncker hana uhakika wa kuungwa mkono kwa wingi na hana haki ya moja kwa moja kwa wadhifa huo wa juu.

Renzi amesema ni muhimu zaidi kulenga wenye agenda ya kisiasa ya halmashauri hiyo badala ya nani apewe wadhifa gani.

Mgombea atakayefanikiwa kushika wadhifa huo anahitaji sio tu kuungwa mkono kwa wingi na bunge la Ulaya bali pia na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Merkel ambaye idhini yake inaonekana kuwa muhimu kwa mgombea,wiki iliopita alimuunga mkono Juncker kushika wadhifa huo.

Pamoja na Uingereza,serikali za Hungary,Sweden na Uholanzi zimeelezea wasi wasi wao juu ya uwezekano wa wadhifa huo kushikwa na Juncker.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters
Mhariri: Oumilkher Hamidou

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com