Jumuiya ya kimataifa yalaani mapinduzi ya Mali | Matukio ya Afrika | DW | 23.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jumuiya ya kimataifa yalaani mapinduzi ya Mali

Jumuiya ya kimataifa inaendelea kuyalaani mapinduzi ya kijeshi ya Mali huku hatima ya Rais Amadou Toumani Toure ikiwa haijulikani na waasi wa Tuareg wa kaskazini mwa nchi hiyo wakisonga mbele kuelekea kusini.

Kikundi cha wanajeshi wa Mali kilichomuondoa madarakani Rais Amadou Toure.

Kikundi cha wanajeshi wa Mali kilichomuondoa madarakani Rais Amadou Toure.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia kwa rais wake wa sasa, Balozi wa Uingereza Mark Lyall Grant, limewataka wanajeshi waliofanya mapinduzi hayo kuurudisha utawala wa kidemokrasia na wao kurudi makambini mwao mara moja.

"Wajumbe wa Baraza la Usalama linalaani vikali uchukuwaji wa madaraka kwa nguvu kutoka serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Mali na baadhi ya wanajeshi wa nchi hiyo. Baraza linawataka wanajeshi hao kuhakikisha usalama wa Rais Amadou Toumani Toure na wao kurudi makambini kwao." Alisema Grant.

Mara baada ya wanajeshi kujitangazia kuchukuwa madaraka hapo jana, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ilitoa tamko la kulaani kitendo hicho na kuapa kutokivumilia.

Ufaransa, kwa upande wake, imesitisha kwa muda ushirikiano wake na koloni lake hilo la zamani na kuwataka wanajeshi kutokumdhuru Rais Toure. Marekani, ambayo mara kadhaa imerejelea wasiwasi wake kwamba baadhi ya sehemu za Mali na nchi jirani zinakuwa eneo falama kwa makundi ya wapiganaji wa Jihadi, imetaka "kurudishwa haraka kwa utawala wa kikatiba."

Lakini msemaji wa wanajeshi waliochukuwa madaraka, Luteni Amadou Konare, alisema hapo jana kuwa mapinduzi yao yalikusudiwa hasa kurudisha utawala wa kidemokrasia kutoka utawala uliofeli kulilinda taifa.

"Lengo letu si kubakia madarakani, bali kuirudisha serikali kwa rais atakayechaguliwa kidemokrasia, kulinda umoja na heshima ya taifa." Alisema Luteni Konare alipokuwa akisoma tamko la mapinduzi kwenye televisheni ya taifa.

Amri ya kutotoka nje

Rais Amadou Toumani Toure.

Rais Amadou Toumani Toure.

Mtu ambaye mpaka sasa anaonekana kuwa ndiye kiongozi wa mapinduzi hayo, Kapteni Amadou Sanogo, ametangaza amri ya kutotoka nje nyakati za usiku na kufungwa kwa mipaka yote ya nchi hiyo hadi hapo kutakapotolewa tangazo jengine. Amewataka pia wafanyakazi wa serikali kurudi kazini Jumanne ijayo.

Wanajeshi walioasi katika mji wa kaskazini mashariki wa Gao wamewaweka kizuizini wakuu wao, wakiunga mkono mapinduzi hayo, huku katika mji mkuu, Bamako, kuna taarifa za wanajeshi kuvamia na kuiba mali na magari ya watu.

Bado haijuilikani kwa kiwango gani hasa kundi la wanajeshi lililojitangazia kufanya mapinduzi hayo lina nguvu, na ikiwa kweli Rais Toure amejisamilisha au amekamatwa.

Chanzo kimoja jeshini, kimeliambia shirika la habari la AFP, kwamba rais huyo yupo mjini Bamako, na wala hakukimbilia ubalozini, kama ilivyokuwa imevumishwa. "Yuko kwenye kambi ya kijeshi na yupo madarakani. Kikosi maalum cha 'Red Beret' kinafuatilia mambo yote." Alisema mwanajeshi huyo aliyekataa kutajwa jina.

Waasi wasonga mbele

Wachungaji wa jamii ya Tuareg.

Wachungaji wa jamii ya Tuareg.

Wakati hayo yakiendelea, waasi wa Tuareg kaskazini mwa nchi hiyo waaripotiwa kuchukuwa maeneo yaliyowachwa na vikosi vya serikali. Wakitumia fursa ya machafuko yaliyopo serikalini hivi sasa, waasi hao wa MNLA wanasonga mbele kuelekea kusini.

Afisa mmoja katika mji wa kaskazini wa Kidal, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba waasi wameichukuwa kambi ya kijeshi ya Anefis, iliyo umbali wa kilomita 100 kuelekea kusini magharibi, baada ya wanajeshi wa serikali kujiondoa.

Katika mji mwengine wa Timbuktu, shahidi ameiambia Reuters kwamba wanajeshi wameondoka hapo na kurudi mji wa Gao na kwamba sasa hakuna uongozi wa kijeshi, akiongeza kwamba karibuni waasi watakamilisha kuichukua miji ya kaskazini.

Uasi huu wa jamii ya Tuareg, ambayo ilinasibishwa sana na utawala ulioondoshwa madarakani nchini Libya, ndio hasa unaotajwa na wanajeshi walioasi kuwa sababu ya mapinduzi dhidi ya Rais Toure, ambaye wanamlaumu kutokuushughulikia vyema. Mamia ya watu wameshauwa katika mapigano kati ya waasi na wanajeshi na maelfu ya wengine wameyakimbia makaazi yao katika miji ya kaskazini ya Mali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman