1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jose Mourinho "arejea nyumbani"

3 Juni 2013

Jose Mourinho ameteuliwa kwa mara nyingine tena kama kocha wa klabu ya Chelsea ya England. Hii ni baada ya uvumi wa miezi sita kuhusiana na kurejea mreno huyo uwanjani Stamford Bridge

https://p.dw.com/p/18j2k
Real Madrid's Portuguese coach Jose Mourinho looks on before the UEFA Champions League semi-final second leg football match Real Madrid CF vs Borussia Dortmund at the Santiago Bernabeu stadium in Madrid on April 30, 2013. AFP PHOTO / JAVIER SORIANO (Photo credit should read JAVIER SORIANO/AFP/Getty Images)
Jose MourinhoPicha: AFP/Getty Images

The Special One, jinsi anavyofahamika amesaini mkataba wa miaka minne. Afisa mkuu Mtendaji wa klabu hiyo Ron Gourlay amesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Chelsea kwamba ana furaha kumkaribisha tena Jose Mourinho.

Habari hizo hazikuwa za kushangaza kwa sababu Mourinho tayari alikuwa amekiambia kituo kimoja cha televisheni nchini Uhispania kuwa atakua kocha wa Chelsea kwa mara nyingine kwa sababu alikuwa na maisha mazuri jijini London na anahisi kuwa watu pale wanampenda.

Bayern yasheherekea historia

Kwa kweli hali ya hewa siyo shabiki wa Bayern Munich, kwa sababu kulikuwa na mvua kubwa na baridi kali iliyotanda mjini Munich wakati mashabiki 10,000 wa Bayrn walipojitokeza mitaani kusheherekea ushindi wao wa kihistoria wa mataji matatu katika msimu mmoja.

Wachezaji wa Bayern wakiwaonyesha mashabiki mataji yao yote matatu waliyoyashinda msimu huu
Wachezaji wa Bayern wakiwaonyesha mashabiki mataji yao yote matatu waliyoyashinda msimu huuPicha: Reuters

Ushindi wa Bayern wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya VfB Stuttgart katika fainali ya komble la Shirikisho la Ujerumani, iliyochezwa Jumamosi, ulikamilisha msimu wao baada ya kushinda mataji ya Champions League na Ligi ya Ujerumani - Bundesliga. Sasa Bayern ndio timu ya kwanza ya Ujerumani kushinda taji la Ulaya, ligi ya nyumbani na kombe la shirikisho katika msimu mmoja, wakati Bundesliga ikiadhimisha mwaka wake wa 50.

Nyota wa Ujerumani Bastian Swcheinsteiger alinyanyua kombe la Shirikisho la Ujerumani, nahodha Philipp Lahm akabeba taji la Bundesliga waakti kocha Jupp Heynckes akipewa heshima ya kunyanyua komble la Champions League. Heynckes mwenye umri wa miaka 68 atakuwa na mkutano wa waandishi wa habari hapo kesho ili kufichua mipango yake ya siku za usoni wakati kocha wa zamani wa Barcelona Pep Guardiola akichukua usukani wa mabingwa hao wa Ulaya mnamo Juni 26.

Mario Gomez anaondoka?

Na wakati sherehe hizo zikiendelea, mshauri wa Mario Gomez amepuulizia mbali ripoti kuwa mshambuliaji huyo wa Ujerumani anatarajiwa kuihama Bayern na kujiunga na Napoli nchini Italia, akisema kuwa hakuna chochote kilichofikiwa. Uli Faerber ameliambia shirika la habari la ujerumani DPA kuwa kwanza watazungumza na Bayern wiki hii. Mshauri huyo amethibitisha nia ya Napoli kumtaka Gomez, lakini akasema hakuna mazungumzo wala makubaliano yaliyofanywa kufikia sasa.

Mario Gomez alifunga mabao mawili katika fainali ya Jumamosi ya DFB Pokal dhidi ya VfB Stuttgart
Mario Gomez alifunga mabao mawili katika fainali ya Jumamosi ya DFB Pokal dhidi ya VfB StuttgartPicha: Reuters

Gomez ni mchezaji wa pili kuhama Bayern baada ya miamba hao kuthibitisha jan kuwa gwiji wao wa Ukraine Anatoly Tymoshchuk atarudi katika klabu aliyokuwa ya Zenit St Petersburg. Tymoshchuk mwenye umri wa miaka 34 amesaini mkataba wa miaka miwili kuanzia msimu ujao na klabu hiyo ya Urusi.

Marekani yaibwaga Ujerumani

Timu ya taifa ya soka ya Ujerumani ambayo haikuwa na wachezaji wake nyota imefungwa magoli manne kwa matatu na timu ya Marekani ambayo inafunzwa na kocha Mjerumani Juergen Klinsmann. Nahodha wa Marekani Clint Dempsey alitikisa wavu mara mbili huku Jozy Altidore akiifunga Marekani jingine pamoja na bao la kuzawadiwa walilojifunga wajerumani. Mabao ya Ujerumani yalifungwa na Hieko Westermann, Marx Kruse na Julian Draxler.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löw, ambaye alifanya ziara fupi ya kucheza mechi mbili nchini Marekani bila ya nyota wowote kutoka washindi wa Champions League Bayern Munich, na waliomaliza wa pili Borussia Dortmund au Rea Madrid, amesema kuwa Marekani walistahili ushindi huo. Ujerumani iliizaba Equador mabao manne kwa mawili katika mechi yao ya kwanza siku ya Jumatano. Katika mchuano mwingine wa kirafiki na ambao ulikuwa wa kuvutia, wenyeji Brazil walitoka sare ya mabao mawili kwa mawili na England katika uwanja wa Maracana mjini Rio de Janeiro.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman